Wabunge, wananchi tuelekeze nguvu zetu kwa wasiolipa kodi

17May 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wabunge, wananchi tuelekeze nguvu zetu kwa wasiolipa kodi

WAKATI Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 ukiendelea, wabunge wamejitokeza kupaza sauti zao zinazoitaka serikali ya Dk. John Pombe Magufuli itimize jukumu lake la kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Miongoni mwa kero hizo ni ile ya maji ambayo kadri ya kilio cha wawakilishi hao wa wananchi, inaonekana bado ni kubwa ingawaje kuna jitihada zinaendelea kuchukuliwa na serikali zikilenga kulimaliza.

Wabunge wengi wamekiri kwamba bado ile ahadi ya Dk. Magufuli kuwatua ndoo akina mama nchini haijatekelezwa ipasavyo.

Na kwamba kama hali ya kusuasua itaendelea katika mtiririko mzima wa kupeleka fedha za miradi ya maji kwa wananchi, kazi ya kuondokana na kero hii itakuwa ngumu.

Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye na Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga ni miongoni mwa waliojitokeza kupaza sauti zao wakiitaka serikali ichukue hatua za kulimaliza tatizo hili.

Na wengine kama Nnauye wakaenda mbali zaidi kukionya chama chao kuwa kama ahadi ya kuwatua wanawake ndoo za maji ambayo iliahidiwa na Dk. Magufuli wakati wa kampeni za urais mwaka 2015 haitatekelezwa, basi huenda wananchi wasikirudishe Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani mwaka 2020.

Ukiangalia sauti hizo za wawakilishi wakati walipokuwa wakijadili bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2017/2018 iliyowasilishwa na Waziri wa wizara hiyo Gerson Lwenge, utaona kwa ujumla zilikuwa zinastahili.

Zilikuwa zinastahili pamoja na pengine kuwa na ‘lengo la kisiasa ndani yake’ kwa sababu ya kupigania jambo jema, kwani upatikanaji wa huduma ya uhakika ya maji kwa wananchi katika umbali unaokubalika ni kwa maslahi ya taifa kwa ujumla wake.

Na ninapoongelea umbali unaokubalika ninarejea ule ulioainishwa kwenye Sera ya Maji ya Taifa ya Mwaka 2002, inayotaka wananchi kufikiwa na huduma hiyo ndani ya mita 400 vijijini na mita 300 mijini na kwa muda usiozidi nusu saa.

Pamoja na mambo mengine, wabunge waliipinga bajeti iliyowasilishwa ya kiasi cha shilingi bilioni 672.2 kwa sababu walidai kuwa ni ndogo ikilinganishwa na ya mwaka unaomalizika wa 2016/2017, iliyokuwa ya Shilingi bilioni 915.

Katika mantiki ya kawaida Muungwana anaona wabunge wana hoja, kwamba kwa nini fedha za bajeti ya maji zipungue mwaka huu, wakati tatizo la maji bado kubwa kwenye maeneo mbalimbali na hasa vijijini!

Lakini wakati Muungwana akiungana na wawakilishi hao kuipigania bajeti ya maji ili itengewe fedha za kutosha kwa lengo la kuondoa kero hii kwa wananchi, anadhani kuna sauti ya pamoja inayopaswa kupazwa na wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla wao.

Muungwana anaona kuwa wabunge na wananchi wanapaswa kuelekeza nguvu zao kwa wananchi wanaostahili kulipa kodi ambao kimsingi hawafanyi hivyo.

Safu hii inaona hili ni la msingi zaidi kwa sababu kodi inayolipwa na wananchi ndiyo kwa sehemu kubwa inayoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, ikiwamo miradi la maji.

Kwamba iwapo kodi ya kutosha itakusanywa kutoka kwa wananchi wote wanaostahili kuilipa, basi suala la kuilalamikia serikali kwa nini haikutenga fedha za kutosha kwenye bajeti ya maji halitakuwapo.

Ninasema hivyo kwa sababu, hata ukiangalia mtiririko mzima wa fedha za miradi ya maji zilizotolewa kwa mwaka 2016/2017, kati ya bilioni 915
zilizopitishwa kufikia Machi mwaka huu, ni asilimia 19.8 tu ya fedha hizo ndizo zilizokuwa zimetolewa.

Mojawapo ya sababu ya msingi ya mapungufu hao inaweza kuwa ni mapato yasiyotosheleza.

Ni kwa maana hiyo Muunganwa anaona ipo haja sasa kwa wabunge na wananchi kwa ujumla kupaza sauti zao ili wananchi wasiotimiza wajibu wao wa kulipa kodi wafanye hivyo kwa dhamira ya kuiwezesha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya maji iweze kutekelezwa kama ilivyopangwa.