Twataka bingwa wa haki

13May 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Twataka bingwa wa haki

NENO ‘chauchau’ lina mana mbili. Kwanza ni kitu anachotoa mtu kwa mwingine ili apate upendeleo; rushwa, mrungura/mlungula.

Maana ya pili ya ‘chauchau’ ni –enye kuchauka au kukosa utaratibu. ‘Chauka’ maana yake ni ‘kazana’ na ‘chaukana’ ni kitendo cha mke na mume au mtu na rafiki yake kutengana.

Tutoke kwenye msamiati (jumla ya maneno yaliyo katika lugha), tuingie kwenye mada yaani undani au kiini cha jambo linalozungumzwa au kujadiliwa. Mada yangu ya leo ni tahadhari kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Takukuru kuhusu uwezekano wa mechi za Ligi Kuu Bara kutekwa na chauchau.

Mpaka sasa zimesalia mechi chache sana kufikia tamati ya Ligi Kuu inayozikutanisha timu 16 nchini kuwania taji hilo maarufu. Ni Simba na Yanga tu kati ya 16 ndizo zinazofukuzana kutwaa ubingwa huo msimu huu.

Imekuwa paka akitoka, panya anatawala. Yupi paka na nani panya, tutaelewa siku chache zijazo.

Yanga imebakiza mechi mbili (mmoja wa kiporo) wakati Simba ikiwa na mechi moja kukamilisha mbio hizo kabla ya michezo yao ya jana Ijumaa kwa Simba na leo Jumamosi kwa Yanga. Lolote laweza kutokea kwani kandanda ni mchezo wa makosa na bahati.

Timu hizo kongwe zenye upinzani wa jadi, huombeana mabaya na kuhasimiana kila mara. Kisa ni gozi la ng’ombe wasilojua nyama kala nani! Kwa ufupi zimekaliana ‘mguu-kausha’ kama walivyo Waarabu na Wayahudi!

Wakati Yanga yataka kurejesha ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo na kulitwaa Kombe hilo moja kwa moja, Simba yataka kuondoa nuksi (kisirani) ya kulikosa kwa misimu minne mfululizo.

Hapa ndipo penye ‘kirumbizi’ yaani ngoma inayochezwa na wachezaji inayohusisha kupigana kwa fimbo. Kwa hali hii, kutakuwa na ‘michezo’ ya nje ya uwanja kutafuta ushindi kwa kile kisemwacho ‘mwenye kisu kikali ndiye alaye nyama’.

Baada ya hapo ngebe (maneno mengi yenye jeuri) za mashabiki zitaenea mitaani. Utadhani wametwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika!

Ninaposema ‘michezo’ ya nje ya uwanja maana yake ni waamuzi kuonwa (nadhani naeleweka). Kadhalika viongozi na wachezaji wanaothamini fedha kuliko hadhi zao na heshima ya vilabu vyao bila kuwasahau waganga na waganguzi. Kumbe wakale wapi? Wajinga ndiwo waliwao bwana!

Kwa upande mwingine kuna timu zilizojihakikishia kushuka daraja. Baadhi ya wachezaji wa timu hizo watakuwa tayari kupoteza mechi zilizobaki kama wakilainishwa kwa ‘sabuni ya roho.’ Inapokuwa hivyo, hakuna starehe ya mashindano!

Badala ya watazamaji kufurahia mchezo, watakuwa kama wanaoangalia ‘lelemama’ yaani ngoma ya wanawake wa Pwani ichezwayo juu ya mabao kwa kutumia mbiu (pembe anayochukua mwanamke kwenye mchezo wa lelemama au bomu).

Nimeeleza haya yote ili kuwazindua viongozi wa TFF, Takukuru na vilabu sawia (kwa wakati mmoja). Wanatakiwa kuwa macho katika hili.

Mara nyingi kesi zinazohusu rushwa michezoni, hasa kandanda, huchukua muda mrefu sana kutolewa uamuzi. Wakati mwingine hata uamuzi unaotolewa huacha maswali mengi yasiyo na majibu ya kuridhisha!

Wahenga walisema “Fedha ilivunja nguu, milima ikalala.” Maana yake Fedha zina uwezo wa kuivunja milima na vilima. ‘Nguu’ ni mlima mkubwa mrefu.

Methali hii hutumiwa kupigia mfano uwezo wa fedha. Mtu akiwa na fedha anaweza kufanikiwa kufanya mambo ambayo asingeweza kuyafanya wala kudhania kuyafanya.

Pia twaambiwa “Fedha fedheha” kwamba pesa huweza kuleta mambo ya aibu baina ya binadamu. Twaonywa kuhusu maovu yanayoweza kusababishwa na pesa.

Waingereza wana usemi usemao “money makes the mare go” yaani fedha ni motisha ya mambo. Twataka ushindi wa haki si wa hela.
[email protected]
0715/0784 33 40 96