Trafiki wasifanye kazi ya taa za kuongoza magari

19May 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Trafiki wasifanye kazi ya taa za kuongoza magari

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alikaririwa hivi karibuni bungeni akisema kuwa bado kuna haja ya trafiki kuongoza magari kwenye makutano ya barabara, pamoja na hatua hiyo kulalamikiwa na baadhi ya watu.

Masauni alisema askari hao wamekuwa wakilalamikiwa kwamba wanasababisha foleni kwa kuingilia kazi ambayo ingefanywa na taa za kuongozea magari zilizo kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na miji mingine.

Akataja sababu zinazowafanya trafiki waendelee kuwapo katika maeneo yote ya makutano ya barabara kuwa ni kutokana na mfumo wa muda mrefu uliowekwa kwenye taa za kuongozea magari, ambao hauendani na wingi wa magari uliopo sasa.

Pamoja na ukweli wa alichosema kiongozi huyo, ninadhani wakati umefika wa kuziboresha taa za barabarani ili zifanye kazi kulingana na mazingira ya sasa kuliko kuendelea kuwatumia trafiki ambao wameonekana kuwa kero kwa baadhi ya abiria na madereva wa magari.

Kimsingi askari wanapaswa kuwa pembeni wakiangalia madereva wanaofanya makosa ya barabarani.

Hilo likifanyika nina imani linaweza kuwaepusha na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo zikiwamo za kutukanwa na wakati mwingine hata kupigwa kwa sababu ya kuchelewa kuruhusu magari kupita.

Kumeripotiwa tukio la trafiki kupigwa kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, kwa sababu tu ya kuchelewesha msafara.

Wakati mwingine trafiki wamejikuta wakipata ajali kutokana na jinsi wanavyosimama katikati ya barabara huku magari yakipita nyuma na mbele yao.

Hali huwa ni tete asubuhi na jioni wakati wakazi wa jijini wakielekea katika shughuli zao za kila siku au kurudi nyumbani, ambapo hukwama kwa muda mrefu kwenye makutano ya barabara, hasa panapokuwapo trafiki akiongoza magari.

Kitu ambacho huwa tofauti pale taa zinapoachwa zifanye kazi na wao wafuatilie madereva wanaofanya makosa.

Tuna madereva wengi wasiozingatia taratibu na sheria za usalama barabarani.

Ninajua zipo sababu nyingine zaidi zinazochangia kuwapo kwa foleni kama vile; ubovu wa mipango miji, kukosekana kwa barabara mbadala hali inayosababisha magari kurundikana sehemu moja.

Aidha, suala la baadhi ya barabara kugeuzwa kuwa maegesho ya magari,
kukosekana kwa barabara za juu ambazo sasa zimeanza kujengwa kwenye baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, pia ni sababu ya kuwapo kwa foleni zisizoisha.

Lakini kubwa zaidi, Muungwana haoni ni kwa nini trafiki alazimike kushinda barabarani ili kuruhusu magari zaidi ya upande mmoja wakati wa kwenda asubuhi na wakati wa kurudi jioni wakati kuna taa!

Mwaka juzi, wachumi walitoa ripoti ikionyesha kuwa Tanzania inapoteza Sh. bilioni 4 kila siku kutokana na foleni, hivyo ni vyema hatua za haraka zichukuliwe kuokoa pesa hizi zinazopotea.

Miongoni mwa hatua ambazo Muungwana anaziona zinafaa ni pamoja na ya kuwaondoa trafiki katika suala la kuongoza magari hali inayochangia foleni zisizo za lazima kutokana na kuruhusu magari ya sehemu moja kwa muda mrefu huku upande mwingine ukielemewa na wingi wa magari.

Taa za kuongozea magari ziko kitaalamu ili kuhakikisha kwamba kila upande unapata nafasi ya kupitisha magari kwa wakati na ndiyo maana kwenye makutano ya barabara ambayo trafiki hawapo huwa hakuna foleni kubwa ya magari.

Wito wangu ni kwa mamlaka kutafakari ninalopendekeza na kisha kuchukua hatua ili kuwasaidia wakazi wa jiji wasiendelee kuteswa na foleni ambazo wakati mwingine siyo za lazima.