Sababu zinazoweza kumkimbiza mteja

12May 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Sababu zinazoweza kumkimbiza mteja

UMESHAWAHI kujiuliza kwa nini biashara yako haifanikiwi, inakufa au inazidi kupoteza wateja siku hadi siku ?

Au umeshawahi kujiuliza kwa nini duka la jirani yako linapata wateja wengi na baadhi yao ni wale waliokuwa wateja wako?

Katika makala haya tutaangalia ni sababu zipi zinazoweza kusababisha kumpoteza au kumkera mteja wako.

Kwa kujua hizo sababu na kuziepuka unaweza kabisa kuongeza wateja, kuwashawishi na kuwarudisha wale uliowapoteza.

Kwanza hakikisha unafungua biashara yako kwa muda unaotakiwa.
Kuna tabia ya baadhi ya wamiliki wa biashara kuchelewa kufungua biashara zao, muda ambao mteja anahitaji kupata huduma.

Sababu hii inaweza kumpoteza mteja au kumkera.

Jenga mazingira ya wewe kumsubiri mteja badala ya yeye kukusubiri sehemu ya biashara yako.

Unapokuwa umeamua kufanya biashara ifanye siku zote ulizojipangia kufanya, kama ni kila siku au kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa basi hakikisha siku hizo unafungua.

Usifanye biashara kwa mazoea au kujisikia kwa mfano, leo unaweza kufungua kesho ukafunga bila sababu za msingi.

Tabia hii inaweza kumsababishia mteja kupata kero na kukuhama kabisa.
Usifungue biashara kwa vile unajua siku fulani kuna wateja na kufunga kwa vile unajua siku fulani hakuna wateja.

Usiwe na tabia ya kufungua biashara na kuacha peke yake na kuzungukazunguka au kwenda sehemu mbali na biashara yako kupiga stori.

Hata kama duka liko wazi mteja anapokuja anatakiwa asipate taabu ya kumtafuta mtoa huduma.
Kuna wateja wengine wanajali muda, hivyo huwa hawana muda wa kupoteza kumsubiri mtoa huduma.

Fikiria kama kuna sehemu nyingine ambapo mteja huyu anaenda na kumkuta mtoa huduma, ataweza kushawishika tena kurudi kwako?

Unatakiwa uwe na kauli nzuri ambayo itamvutia mteja kuja kwako kupata huduma siku nyingine.
Kauli nzuri na yenye staha huwa ni asali kwa mteja.

Kuna wateja wengine ndio wanaweza kuwa na kauli mbaya, lakini wewe hupaswi kumjibu mteja kwa lugha ile.

Kumbuka wewe ndiye unayetafuta na siyo mteja.

Soma saikolojia ya mteja wako, mhudumie kwa upendo na ukarimu wa hali ya juu ili siku nyingine arudi tena.
Kwa hiyo kauli mbaya ni moja ya sababu ambazo zinaweza kukuletea matokeo hasi katika biashara yako.

Ipende biashara yako, kwa kuwa ndiyo kazi uliyochagua kuifanya.

Kuna wafanyabiashara wengine huwa wanatoa huduma kama vile wamelazimishwa.

Kutopenda kazi yako ni moja ya sababu zitakozomfanya mteja naye asivutiwe na biashara yako.

Kuwa na uso wa furaha, mchangamkie mteja, ongea naye vyema katika lugha ya ushawishi, onyesha jinsi gani unaipenda kazi yako.

Unapofanya biashara kwa moyo na juhudi zote huwezi kumpoteza mteja.

Kwa hiyo ili ufanikiwe katika biashara au jambo lolote lile, kwanza penda hicho unachokifanya na mwingine atakipenda.

Usiwe na tabia ya kubadili bei mara kwa mara au kuongeza bei kuliko bei ya kawaida.

Kuna baadhi ya wafanyabiashara wanauza vitu kwa bei ya juu sana ili kupata faida kubwa.

Hapa unakuwa unamlangua mteja na kumkatisha tamaa tena ya kurudi kwako.

Pia unapofanya biashara usiwe mtu wa kubadilisha bei mara kwa mara, leo mteja akija bei hii, kesho bei nyingine, hali hiyo itamfanya akose imani na wewe na kukukimbia kabisa.

Ya mwisho na ninayodhani ni sababu kubwa, ni kuhama au kuhamisha sehemu ya biashara bila kutoa taarifa kwa wateja. Hii itakufanya kupoteza karibu wateja wote.

Jenga tabia ya kutoa taarifa mapema kama una mpango wa kuhamisha biashara au kubadili biashara.

Kwenye taarifa yako onyesha wapi ulikohamia au ni biashara ipi unataka kuongeza au kubadili.

Hizi ni baadhi tu ya sababu ambazo zinaweza kuwa kero au kumpoteza mteja katika biashara yako.

Kama wewe ni mfanyabiashara na una tabia kama hizi chukua hatua mara moja na utaona mabadiliko katika biashara yako.