Maendeleo ya watoto shuleni yawe sehemu ya maisha ya wazazi

23Feb 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Maendeleo ya watoto shuleni yawe sehemu ya maisha ya wazazi

WAZAZI ni wadau muhimu katika sekta ya elimu na wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kuiboresha, iwapo watatambua kwamba wanatakiwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.

Lakini ni bahati mbaya, baadhi yao wamebweteka na kudhani jukumu ni la walimu pekee. Wao hawana nafasi ya kutoa ushirikiano. Ni hali inayosababisha kukosekana kwa mawasiliano kati ya pande hizo mbili, ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya kielimu kwa mtoto.

 

Mfano mmojawapo wa kuwapo kwa hali hiyo, ni malalamiko ya hivi karibuni yaliyotolewa na baadhi ya walimu na wazazi wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi, walipojadili changamoto za sekta hiyo.

 

Walimu na wazazi hao walisema hayo kwa nyakati tofauti katika mikutano mbalimbali iliyoandaliwa na asasi ya Kuunganisha Vijana Kimaendeleo Ruangwa (Akuvikiru), kwa ajili ya uwasilishaji taarifa za mradi wa maboresho ya elimu ya sekondari.

 

Mbali na hilo, waliongeza kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaelekeza watoto wao kufanya vibaya katika mitihani, ili mwisho wa siku wasifaulu wabaki nyumbani wakisubiri ama kuoa au kuolewa.

 

Nimetoa mfano wa Ruangwa, kwa sababu nilikuwapo kwenye tukio mojawapo. Lakini, ninaamini changamoto kama hizo zipo karibu nchi nzima, kwani zimekuwa zikiripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.

 

Hivyo ni muhimu kuwakumbusha wazazi wenye tabia hiyo, kwamba mtoto hujifunza kupitia shule za aina tatu kuanzia elimu isiyo rasmi, ambayo inajumuisha maelekezo ya msingi na malezi kutoka kwa wazazi wenyewe au walezi.

Shule hiyo ambayo walimu wake ni wazazi ni msingi muhimu katika makuzi na maendeleo ya mtoto na akitoka hapo anaingia shule ya pili inayojihusisha kuiga matendo ya wazazi wake kimya kimya na kujaribu kufanya kama wanavyoongea au wanavyofanya.

 

Iwapo mmoja wa wazazi atakuwa ni mtu wa kupenda kupiga kelele, mtoto naye ataiga kimya kimya. Iwapo atakuwa mtu wa kutukana, mtoto naye ataiga kimya kimya na kama atakuwa mwenye tabia njema, naye ataiga hivyo.

 

Wazazi na walezi ni watu wa muhimu katika makuzi ya mtoto. Anapokuwa katika shule hizo mbili katika makuzi yake, mtoto anapoingia shule ya tatu, ili afanye vizuri, huku wao wakifuatilia maendeleo yake.

 

Hapa ndipo katika nazungumzia elimu rasmi, ambayo mtoto anajumuika na wenzake shuleni, lakini bahati mbaya baadhi ya wazazi wanatuhumiwa kushindwa kutimiza moja ya wajibu wao wa kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni.

 

Kama nilivyosema, wazazi na walezi ni watu muhimu katika jamii, wanaoweza kuwasaidia watoto kufikia ndoto zao, wakitambua kwamba wao ni walimu wa kwanza kwa mtoto kuanzia nyumbani hadi shuleni.

 

Vilevile, wazazi na walezi ndiyo wenye jukumu la kumjenga na kumwandaa mtoto, ili awe wa aina fulani, kwani kwa ujumla watoto wanapenda kuiga tabia za wazazi au walezi wao na watu wengine wanaowazunguka kwenye makuzi yao.

 

Wakati walimu wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha watoto wanajua kusoma na kuandika vizuri, wazazi nao wanapaswa kuwaunga mkono kwa kuwahimiza watoto kusoma kwa bidii badala ya kuwaacha wafanye wanavyotaka.

 

Mbali na hilo, wazazi wanatakiwa kuwatia moyo walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya, huku wakitambua kwamba walimu ni wazazi pili, ambao ni vyema kuwa nao karibu ili kupata taarifa za maendeleo ya watoto wao shuleni.

 

Iwapo wazazi na walezi wakashiriki kikamilifu katika suala zima la elimu kwa watoto wao itakuwa ni rahisi kujua changamoto zinazowakabili na hata linapotokea tatizo kama utoro au utovu wa nidhamu kwa ujumla inakuwa ni rahisi kulitatua kwa pamoja.

 

Ushirikiano baina ya walimu na wazazi na kuwapo kwa mawasiliano ya mara kwa mara ni jambo la msingi sana katika maendeleo ya mtoto shuleni kwa sababu vinasaidia kupandisha kiwango cha elimu.

Wazazi wana mchango mkubwa katika kuwatokomeza maadui watatu, maradhi, ujinga na umaskini, waliotangazwa na serikali mara tu baada ya nchi hii kupata uhuru mwaka 1961.

 

Maadui hawa wanaweza kutokomezwa iwapo elimu ikizingatiwa, kwani ndiyo mkombozi pekee katika maisha, hivyo wazazi na walezi wasiozingatia jambo hili watafakari na kisha wachukue hatua, vinginevyo maadui hao wataendelea kujichimbia nchini.

 

Kwa hiyo, ni vyema wakatambua wajibu au majukumu na kazi zao kwenye malezi ya watoto wakizingatia kuwa elimu ni msingi mkubwa katika kumkuza na kumwelekeza mtoto akue kwa kufuata maadili mema.