Kila mtu anafaa kuwa dereva wa mabasi ya shule?

18May 2017
Jackson Kalindimya
Nipashe
Mjadala
Kila mtu anafaa kuwa dereva wa mabasi ya shule?

Je, kila mtu anastahili kuwa dereva wa magari ya shule na abiria? Dereva ni kila anayeendesha gari barabarani? Madereva wa mabasi ya shule wanafundishwa wapi na mafunzo yao yanasimamiwa kikamilifu ili kuwawezesha kupata ujuzi wa kutosha kuendesha magari hayo?

Nimeamua kuchambua suala hili nikitanguliza kuuliza maswali hayo hapo juu, ili kujaribu kuziamsha na kuzifikirisha akili ili zilitazame suala hilo kwa kutumia akili na maarifa yote.

Baadhi ya watu wanaamini kuwa, udereva ni kazi rahisi inayoweza kufanywa na mtu yeyote yule, alimradi anamudu kuliwasha, kuliongoza na kulifanya lisimame sehemu anayojisikia kufanya hivyo.

Mtazamo huu, yawezekana ukawa unaungwa mkono na watu wengi wanaomiliki magari yao au wanaojiandaa kununua ili wayaendeshe kwa uhuru na mbwembwe wanazotaka, kama njia ya kuwathibitishia wengineo kuwa ‘amejikomboa’.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI) inabainisha kuwa dereva ni 1.Mwendeshaji wa vyombo vinavyosafiri nchi kavu kama vile treni, trekta au motokaa 2.Mtu aliyeajiriwa kuendesha gari.

Kwa mtazamo wangu, mtazama huo peke yake hautoshi ni dhana dhaifu sana, katika kumtazama dereva na mazingira anayofanyia kazi.

Dereva lazima awe mtu mwenye akili timamu, macho yanayoona vyema yasiyo na chembe ya shaka, umri unaovuka miaka 18 na ahudhurie mafunzo ya udereva katika vyuo sahihi na kupata ujuzi wa kutosha kuhimili chombo cha moto katika mazingira yenye changamoto nyingi na yale ya kawaida. Awe na nidhamu, asitumie kilevi cha aina yoyote anapoifanya kazi hiyo na awe na hofu ya Mungu.

Dereva mwenye sifa hizo anakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya kazi yake kikamilifu tena kwa uhakika kinyume na yule asiye na sifa hizo.
Yawezekana wanaopewa dhamana ya kuendesha magari barabarani hawana sifa zinazojitosheleza. Wanaendesha tu kwa sababu wanajua kuwasha gari, kuliondoa na kulisogeza toka eneo moja kwenda jingine.

Watu aina hii, ni rahisi sana kusababisha ajali kwa sababu hawana maadili, hawajaiva kikamilifu au kuna matatizo katika milango yao ya fahamu hata kuchangia kusababisha ajali. Hawazingatii alama za usalama barabarani.

Wanakimbiza magari kama kwamba mwisho wa dunia unafikia ukomo wake kesho na hawako tayari kuona watu wanakuwapo baada ya hapo. Matokeo yake wanasababisha vifo kwa watu wasio na hatia, kuzalisha walemavu, kuharibu mali na kuyafanya maisha ya abiria na watembea kwa miguu kuwa ya mashaka matupu .

Hayo yanatokea, wakati sheria za usalama barabarani zipo, pamoja na askari wa usalama barabarani wenye dhamana ya kuhakikisha kuwa, sheria hizo zinazingatiwa nao wapo.

Ajali za barabarani na vyombo vya usafiri kwa ujumla, ni moja ya matukio yanayokatisha maisha ghafla na kusababisha vilio, majonzi na umaskini kwa familia na taifa.

Mengi yamesemwa, mikakati imefanyika na sheria zimetungwa, lakini bado ajali za barabarani zinaendelea kuwa jinamizi linaloendelea kukatisha uhai wa watu wengi nchini.

Hivi karibuni, taifa limejikuta katika maombolezo ya vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vincent ya Arusha, waliokatisha maisha kwa ajali ya barabarani wakati wakielekea Karatu kwenda kufanya mtihani wa majaribio.

Chanzo cha ajali hiyo iliyotokea majira ya alfajiri ya Mei 6, mwaka huu, bado kinafanyiwa uchunguzi. Na bahati mbaya ni kuwa, dereva ambaye angekuwa shahidi muhimu katika uchunguzi huo alikufa katika ajali hiyo.

Yawezekana vitu vingi vikatajwa kuwa, vinachangia ajali za barabarani ikiwamo miundombinu ya barabara na mengineyo.

Pamoja na hayo, yawezekana kuna udhaifu mkubwa katika utoaji wa mafunzo na ajira kwa madereva wa mabasi ya shule. Sio kila mtu anaweza kuwa dereva wa mabasi ya shule hata kama ana leseni inayomruhusu kuendesha magari barabarani.

Lazima kujiridhisha kuwa ana akili timamu, hatumii kilevi cha aina yoyote ile, hana matatizo ya kisaikolojia au msongo wa mawazo na anatambua dhamana halisi ya kuendesha gari la shule kwa vitendo vyake na maamuzi yake pasi na shaka.

Dereva ambaye hana hofu ya Mungu, hana utulivu na hana uwezo wa kukabiliana na changamoto za barabarani hafai kukabidhiwa dhamana hiyo.

Anayeaminia kuwa barabara ni kwa ajili yake na gari lake. Hazingatii usalama wa watumiaji wengineo. Pia asiyeshaulika na mwenye kupenda kukimbiza gari kila wakati hafai.

Dereva anayefaa, ni yule anayezingatia usalama wa gari lake na abiria anaowabeba, msikivu , mvumilivu na mwenye ujuzi mkubwa wa kuendesha magari ya abiria akiwa hana rekodi ya kufanya makosa katika kazi hiyo.

Maombolezo ya kitaifa ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva yaliyofanyika hivi karibuni, yatakuwa na maana sana kama mikakati ya makusudi na ya dhati kabisa itafanywa kuhakikisha kuwa, magari yote ya shule yanakaguliwa mara kwa mara na wakaguzi waliohitimu vyema na wasio na chembe ya shaka ya umakini na uaminifu kwa kile wanachokifanya.

Pia vyuo vinavyotoa mafunzo kwa madereva, lazima viwe vile vinavyotambuliwa na serikali, vyenye walimu waliohitimu vyema na sio bora walimu na vinakidhi vigezo vya kutoa mafunzo hayo.

Eneo la uendeshaji wa magari ya shule lazima liangaliwe kwa uangalifu mkubwa na ikibidi kuwa na leseni maalum kwa wote wanaokadhibiwa dhamana hiyo ili kupunguza kabisa uwezekano wa kutokea ajali za barabarani.