Yanga gusa urushwe

09May 2016
Somoe Ng'itu
Lete Raha
Yanga gusa urushwe

RAHA tupu Jangwani. Naam, mashabiki wa Yanga wameendelea kuwa wenye raha baada ya timu yao kuendeleza desturi ya ushindi kwenye mashindano yote.

Kikosi cha Yanga

Jana, Yanga imeibuka na ushindiwa mabao 2-0 dhidi ya Sagrada Esparanca ya Angola katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mashujaa wa Yanga jana walikuwa ni winga Simon Happygod Msuva na mshambuliaji Matheo Antony Simon waliofunga mabao hayo kipindi cha pili, baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza.

Kwa ushindi huo, Yanga itahitaji sare tu au kufungwa si zaidi ya 1-0 katika mchezo wa marudiano wiki ijayo nchini Angola ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa kutoka Ghana, Joseph Odartei Lamptey aliyepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera David Laryea na Malik Alidu Salifu, Yanga ilipoteza nafasi nyingi za kufunga kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili pia kilianza kwa ugumu, Yanga wakiendelea kutengeneza nafasi nzuri na kushindwa kuzitumia, hali iliyoufanya mchezo uwe mgumu upande wao.
Kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Amissi Joselyn Tambwe ndiye ambaye hakuwa na bahati kabisa siku ya leo kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi.

Baada ya kosakosa za muda mrefu, hatimaye vijana wadogo wazawa, Msuva na Matheo wakawainua mashabiki wa Yanga mfululizo kwa mabao safi.
Msuva alianza dakika ya 72 akimalizia krosi maridadi ya winga Godfrey Mwashiuya aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Malimi Busungu, kabla ya Metheo kufunga la pili dakika ya 90 kwa shuti la mbali.

Pamoja na ushindi huo, Yanga ilionekana kabisa kuathiriwa na kuwakosa nyota wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma ambao walikuwa wanatumikia adhabu za kadi za njano walizopewa mfululizo kwenye mechi dhidi ya Al Ahly mwezi uliopita.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela/Mbuyu Twite dk46, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Malimi Busungu/Godfrey Mwashiuya dk53, Amissi Tambwe na Deus Kaseke/Matheo Anthony dk77.

Sagrada Esperanca; Yuri JKose Tavazes, Roadro Juan da Semero/Paul Camufingo dk64, Dennis Conha Morais, Asenio Cabungula, Antonio da Silva Oliveira/Evanildo de Jesus Pedro dk64, Ntaku Zabakaka, Manuel Paulo Joao, Alentua Tangala Rolli, Osvaldochitumba Palana/Aderito Chosolla dk80, Manuel Sallo Conha na Antonio Kasule.

Habari Kubwa