Simba warejea, macho kwa Mbao

23Feb 2018
Somoe Ng'itu
Nipashe
Simba warejea, macho kwa Mbao

KIKOSI cha Simba kimerejea nchini salama kwa mafungu kikitokea Djibouti walikokuwa wakivaana na wenyeji Gendarmarie Nationale FC katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa sasa itakutana na Al Masry ya Misri katika hatua ya awali baada ya kuiondoa Gendarmarie Nationale FC kwa jumla ya mabao 5-0.

Fungu la kwanza la wachezaji 15 lilitua nchini juzi usiku na kundi la pili lililokuwa na wachezaji watano, viongozi na mashabiki wa timu hiyo waliwasili jana asubuhi.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, aliliambia gazeti hili jana kuwa wamerejea salama na kikosi cha timu hiyo kitaanza mazoezi leo kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC utakaofanyika Februari 26 mwaka huu.

Djuma alisema kuwa mazoezi yao yatalenga mashindano yote mawili ambayo wanashiriki na wanajua umuhimu wa kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili kutimiza malengo waliyoweka msimu huu.

 

Habari Kubwa