Simba: Ubingwa sasa ni muujiza

14May 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Simba: Ubingwa sasa ni muujiza

INAWEZEKANA, lakini miujiza na bahati ndiyo vitu pekee vitakavyoifanya Simba iweze kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2016/17 ambao unatarajiwa kumalizika Oktoba 20, mwaka huu.

Kauli hiyo aliitoa Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, baada ya timu yake kufikisha pointi 65 na ikiwa imebakiwa na mechi moja ya funga dimba dhidi ya Mwadui FC kutoka Shinyanga.

Mayanja alisema mbio za ubingwa msimu huu zilikuwa ngumu na ndio maana hadi jana hakuna timu yenye uhakika wa kutwaa taji hilo na kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani.

Mganda huyo alisema kimahesabu Simba inaweza kutwaa taji hilo, lakini ni lazima mahasimu wao Yanga wapoteze au watoke sare katika mechi zao mbili zilizosalia dhidi ya Toto Africans na Mbao FC ambazo ziko katika janga la kushuka daraja.

"Na hata wakipoteza, bado sisi tulikuwa na changamoto ya kuzidiwa mabao ya kufunga na Yanga, hatuwezi kuwa mabingwa kwa kuangalia tofauti ya mabao na hatuwezi kuwafunga Mwadu mabao 10 katika mechi ya mwisho, ni jambo lisilowezekana, ila lolote linaweza kutokea wacha tuone hadi siku ya mwisho," alisema Mayanja.

Aliongeza kuwa wanawapongeza wachezaji wao kwa kupambana hadi sasa bila kukata tamaa na kuahidi kutopoteza mechi iliyobaki na vilevile kuongeza mikakati ili kushinda mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC utakaofanyika Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Mshindi wa mechi hiyo ya fainali atapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayofanyika mwakani huku bingwa wa Ligi Kuu akienda kuchuana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Habari Kubwa