Pluijm hataki kukata tamaa

23Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Pluijm hataki kukata tamaa

LICHA ya kuachwa kwa pointi nane na vinara wa ligi kuu Simba, Kocha wa Singida United, Hans va der Pluijm, amesema kikosi chake bado kina nafasi ya kutwaa ubingwa na bado hawajakata tamaa.

Kocha wa Singida United, Hans va der Pluijm.

Singida United inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 34 huku ikipitwa kwa pointi tatu tu na Yanga wanaoshika nafasi ya pili na pointi moja nyuma ya Azam wanaoshika nafasi ya tatu.

Akizungumza na Nipashe, Pluijm, alisema kuwa mpaka sasa hakuna timu iliyojihakikishia ubingwa na kwa timu zote zinazoshika nafasi nne za juu zina nafasi sawa kutwaa ubingwa.

"Hakuna timu ambayo tayari imejihakikishia ubingwa, sisi tutaendelea kupambana kwa mechi zetu zilizobakia ili kuona nafasi yetu ya kutwaa ubingwa, naamini tuna nafasi ya kufanya hivyo," alisema Pluijm.

Alisema kwa sasa wanaendelea na maandalizi ya mchezo wao wa kombe la FA dhidi ya Polisi Tanzania utakaochezwa kesho

"Baada ya mchezo huo sasa tutaelekeza nguvu zetu kwenye mchezo wa ligi kuu," alisema.

Mchezo unaofuata wa ligi kuu, Singida United itaikaribisha Azam FC kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida.

Mchezo huo huwenda ukatoa taswira ya timu gani kati ya hizo itakaa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu kutokana na kupishana kwa pointi moja huku zote zikiwa zimecheza michezo 19.  

Habari Kubwa