Clinton: Ajib atatisha PSL

15May 2016
Somoe Ng'itu
Lete Raha
Clinton: Ajib atatisha PSL

KOCHA wa Lamontville Golden Arrows FC, Clinton Paul Larsen, amesema straika wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Ajib, anaweza kucheza timu yoyote ya ya Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini, maarufu kama PSL.

Clinton Paul Larsen kushoto.

Kocha huyo mzaliwa wa Durban, KwaZulu-Natal mwenye umri wa miaka 45, amemuambia wakala Rodgers Mathaba anayemsimamia Ajib kwamba amevutiwa na uchezaji wa mshambuliaji huyo wa Simba SC ya Tanzania.

“Hajib alifunga bao zuri katika siku yake ya kwanza ya majaribio, huo ulikuwa mwanzo mzuri kwake, na siku ya pili alifanya vizuri pia, hakufunga, lakini alisaidia kupatikana bao.

Nimezungumza na kocha Clinton alisema Ajib ni mchezaji mzuri sana anaweza kucheza timu yoyote ya PSL nchini,” alisema Mathaba.

Mathaba amewaalika Watanzania wawili kwa majaribio nchini humo, pamoja na Hajib mwingine ni kiungo chipukizi wa Azam FC, Omar Wayne ambaye tayari amefuzu majaribio katika klabu nyingine ya Ligi Kuu, AmaZulu.

Hata hivyo, Wayne ameambiwa kutokana na umri wake mdogo inabidi asajiliwe kama mchezaji wa kikosi cha pili.

Wayne mwenyewe amesema anaweza kukubali kusajiliwa AmaZulu B, lakini wasiwasi wake ni kama klabu yake, Azam FC itakubali kumtoa bure.

Mathaba sasa anapanga kufanya mazungumzo na uongozi wa Azam FC juu ya Wayne aliyeibukia katika akademi ya klabu hiyo yenye maskani yake Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Baada ya kufanya vizuri katika akademi, Wayne aliyekuwa nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys mwaka jana msimu alitolewa kwa mkopo timu za Ligi Kuu kuanza kupata uzoefu.

Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Wayne alicheza Majimaji ya Songea na mzunguko wa pili akahamia Coastal Union ya Tanga, ambako hata hivyo aliondoka mapema kutokana na mipango yake ya kwenda Afrika Kusini.

Habari Kubwa