Watoto wapewe haki za msingi

16Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Watoto wapewe haki za msingi

TANZANIA leo inaungana na mataifa mengine barani Afrika katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

Maadhimisho ya siku hiyo ni utekelezaji wa azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990, kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa Kitongoji cha Soweto Afrika ya Kusini waliouawa na polisi wa iliyokuwa serikali ya ubaguzi wa rangi ya Makaburu Juni 16, mwaka 1976.

Watoto hao walifanyiwa kitendo hicho cha kinyama kutokana na kuandamana kudai haki zao za msingi walizokuwa wananyimwa ikiwamo elimu bora, hivyo kuupinga mfumo wa elimu ya kibaguzi wa rangi.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto.’ Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya mtoto ili iweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Tunaungana na wadau wengine katika maadhimisho haya tukishauri kwamba serikali na asasi mbalimbali kushirikiana katika kupanga mikakati ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ubaguzi na udhalilishaji ambavyo vinachangia katika kuwanyima haki zao za msingi.

Ni ukweli usiopingika kuwa matukio ya udhalilishaji dhidi ya watoto yamekuwa yakiongezeka yakiwamo ya ubakaji, kulawiti, ndoa za utotoni na mimba kwa watoto wa shule, ukeketaji, ajira mbaya na kukosa fursa ya kupata elimu. Liko tatizo la lishe duni ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa vifo vingi vya watoto chini ya miaka mitano.

Aidha kupitia maadhimisho haya, Serikali na wadau tunawashauri kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto na kuzitafutia ufumbuzi.

Kadhalika ipo haya ya kuyatumia maadhimisho haya kama fursa ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera za taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.

Pamoja na changamoto zilizoko, kwa kiasi fulani serikali imechukua hatua za kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na kuwapatia baadhi ya huduma za msingi na zinapaswa kupongezwa.

Uamuzi wa kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari ni moja ya hatua ambayo imefungua njia na kuwapa fursa watoto wengi wa familia maskini kuandikishwa na kupata elimu, tofauti na awali ambapo ada na michango mingine vilikuwa kikwazo kwao kupata elimu ambayo ni hitaji muhimu na msingi wa maisha.

Kuanzishwa kwa madawati ya kijinsia katika vituo vya polisi nchini kumesaidia sana kurahisisha ufuatiliaji wa matukio ya udhalilishaji wa watoto na kuwakamata watuhumiwa kwa urahisi na hatua kuchukuliwa kwa wakati mwafaka.

Serikali pia imefanya uamuzi mzuri wa kuweka maofisa ustawi wa jamii katika hospitali ambazo zinashughulikia watoto walioathiriwa na matukio ya udhalilishaji wa kuwapa ushauri nasaha pamoja na wazazi wao.

Tunaamini kuwa matukio hayo yataendelea kupungua kwa hususani baada ya serikali kuahidi kwamba inakusudia kupitia upya sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa imepitwa na wakati kutokana na kuwa na kasoro nyingi ambazo zinawaathiri zaidi watoto wa kike.

Kwa kuwa mwaka huu maadhimisho hayo kwa mwaka huu yatafanyika kimkoa, hivyo tunatarajia kila mkoa utaadhimisha siku hii kwa kuweka mikakati na mipango ya kuwalinda watoto ambayo inazingatia mazingira yake.

Habari Kubwa