Waliotajwa ripoti mchanga waipe ushirikiano serikali

13Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Waliotajwa ripoti mchanga waipe ushirikiano serikali

KAMATI ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli Aprili 10 mwaka huu ikiwashirikisha wataalamu wa uchumi na sheria kuchunguza madini yaliyomo kwenye mchanga wenye madini ulio ndani ya makontena yaliyopo maeneo kadhaa nchini, jana iliwasilisha taarifa yake.

Taarifa hiyo ilikabidhiwa kwa Rais Magufuli katika hafla iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Spika wa Bunge, Job Ndugai; Kaimu Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Hamis Juma, mawaziri, wakuu wa vyombo vya dola, viongozi wa dini, vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Nehemiah Osoro, akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya wenzake saba, aliibua madudu mengi yaliyofanywa na viongozi na watendaji wa serikali waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za Taifa, lakini hawakuwajibika, badala yake wakahusika kuisababishia nchi hasara ya matrilioni ya fedha.

Kamati hiyo iliyochunguza athari za kiuchumi, inasema kuanzia mwaka 1998 taifa limepata hasara ya kiwango cha juu cha Sh. trilioni 700 na cha chini Sh. trilioni 300 na fedha zilizopotea zingeweza kujenga na kukamilisha reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Mambo yaliyotajwa ni ukwepaji wa kodi, taarifa za uongo kuhusu usafirishaji wa makinikia, uhujumu uchumi, kulisababishia taifa hasara, baadhi ya watumishi wa umma kujipatia mali kwa njia za udanganyifu na kulitia aibu taifa.

Kutokana na mapendekezo 21 yaliyotolewa na kamati hiyo, Rais Magufuli aliagiza kuhojiwa kwa waliokuwa Mawaziri, makamishina wa madini, wanasheria wa serikali na waliokuwa watumishi katika idara za serikali zilizoruhusu wizi wa madini na kuikosesha serikali mapato.

 Magufuli alitoa maelekezo hayo akionekana kukasirishwa na ripoti hiyo kuhusu masuala ya kiuchumi, kisheria na mikataba ya madini iliyoingiwa na Tanzania kwa kampuni ya Acacia.

 Waliotajwa ni waliowahi kuwa Mawaziri wa Nishati na Madini kwa serikali ya awamu ya tatu, nne na tano, Nazir Karamagi, Marehemu Dk. Abbdallah Kigoda, Daniel Yona, Willium Ngeleja na Prof. Sospeter Muhongo. wanasheria wa serikali ni Andrew Chenge, Johnson Mwanyika, Felix Mrema na Maria Ndosi na makamishina wa Madini, Dk. Dalali Kafumu na Paul Masanja.

Tunakubaliana na mapendekezo ya kamati na kubwa lililotugusa ni la kumwagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Kabudi, kuunda timu ya wanasheria kupeleka muswada wa marekebisho ya sheria hiyo bungeni.

Hilo ndilo jambo ambalo limekuwa likipendekezwa na wengi wenye uzalendo na nchi yetu kuwa sheria ya madini inatoa mianya ya kuibwa kwa madini yetu, hivyo tunaamini sheria hiyo ikienda bungeni itafanyiwa marekebisho na kuwekwa udhibiti katika uchimbaji na usafirishaji wa madini nje.

Tunampongeza Rais Magufuli kwa uzalendo wake uliomsukuma kuahidi kwamba mapendekezo yote ya kamati hiyo yatatekelezwa kwa asilimia 100 na kwamba yako tayari bunge kutumia muda wa ziada kufanya kazi hiyo.

Ni imani yetu pia kwamba Bunge likipelekewa sheria hiyo, wabunge watakubaliana na marekebisho kama serikali itakavyopendekeza kama alivyoahidi Spika Ndugai jana.

Tunawashauri wote waliotajwa katika ripoti hiyo kuisaidia serikali kwa kutoa ushirikiano pale watakapoitwa na kutoa taarifa zitakazohitajika kwa usahahi na kwa kina kwa sababu hatua zinazochukuliwa zina lengo la kuwanufaisha Watanzania na rasilimali zao na kuondokana na umaskini uliowatesa wa miaka nenda rudi.

Habari Kubwa