Vyama vya siasa vipate somo Kigoda cha Nyerere

15Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Vyama vya siasa vipate somo Kigoda cha Nyerere

VYAMA vya siasa Afrika vimepewa changamoto ambayo kama vitaifanyia kazi zinaweza kubadilika na kuwatumikia wananchi.

Msomi mkongwe barani Afrika amevishauri vyama hivyo kubadilika kimfumo na kiundeshaji pamoja na kujiunda upya ili viweze kuleta maendeleo katika nchi zao.

Ushauri huo ulitolewa juzi katika Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Prof. Abdoulaye Bathily, gwiji wa historia kutoka Senegal, wakati akiwasilisha mada iliyohusu mchango wa wanasiasa barani Afrika katika kuinuka ama kuanguka kwa mataifa yao.

Alisema vyama vingi vya siasa vingi vinajiendesha bila kuzingatia malengo ya nchi husika, na vingi huangalia maslahi yao binafsi kuliko mustakabali wa nchi.

Kwa mujibu wa msomi huyo nguli, vyama vingi vya siasa lengo lao kuu ni kumweka madarakani mtu vinayemtaka, ama kwa lugha nyingine ni kushika nchi tu badala ya kuangalia maslahi ya nchi na kwamba hata wakishika nchi wanajiandaa na uchaguzi ujao badala ya kuleta maendeleo.

Alisema Afrika itapata maendeleo kutakapokuwapo na umoja miongoni mwa vyama vya siasa.

Prof. Bathily alibainisha pia kuwa vyama vingi vya siasa barani Afrika vinaendeshwa na watu wachache wenye maslahi binafsi na wengi wao ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya ama biashara haramu.

Alishauri kwamba sasa ni wakati mwafaka wa kuunda upya vyama vya siasa ili viwe kama ilivyokuwa miaka ya zamani ambapo vyama vya siasa vilianzishwa kwa lengo la kuleta ukombozi wa nchi.

Mada ya Prof. Bathily ni shule darasa tosha kwa vyama vingi barani Afrika kwa kuwa vimeondoka katika misingi na malengo ya kuanzishwa kwake.

Jambo la kufurahisha ni kuwa msomi huyo alitolea mada yake katika nchini ambako vyama vingi vinakabiliwa na changamoto zote alizozitaja.

Kimsingi, aliyoyasema yana ukweli kwa asilimia mia moja. Ni ukweli usiopingika kuwa vyama vingi kati ya 22 vyenye usajili wa kudumu ni mali ya watu binafsi na vinaendeshwa na wachache wenye maslahi binafsi.

Kwa takribani miaka 25 ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992, kumekuwapo na utitiri wa vyama, lakini kilichobainika ni vyama vingi kutokuendeshwa kama taasisi na kukosa mifumo, hivyo kuonekana ni mali ya watu binafsi badala ya kuwa mali ya wanachama.

Kutokana na hali hiyo, vyama vingi havina sera, itikadi, malengo na mikakati inayoeleweka. Sababu hizo ndizo zinazovifanya vikose mwelekeo na mwishowe kukimbiwa na wanachama pamoja na kuandamwa na migogoro ya kila uchao.

Ni kweli kwamba vyama vilivyoanzishwa kabla ya uhuru wa nchi za bara hili vilikuwa na malengo hususani ya kudai uhuru na baaadaye kujielekeza katika mipango ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Kuna mambo mengi ya msingi ambayo vyama vingeweza kujielekeza vinaonekana kuwa vinatetea maslahi ya taifa kama kutetea rasilimali za taifa ikiwamo kupinga vitendo vya ufisadi, vita dhidi ya umaskini na kupigania huduma bora za jamii kama elimu na afya.

Tunaamini kuwa mada ya Prof. Bathily itakuwa ni darasa tosha kwa vyama vyetu vya siasa kujibadili kitaasisi, kimfumo na kiuendeshaji ili kukidhi matakwa na matarajio ya wanachama wake.

Ushauri wetu ni kwamba ni mwafaka wa kuanzishavyama vya siasa vyenye malengo ya kuisaidia jamii kama ilivyokuwa miaka ya zamani.

Bila shaka wasomi wetu ambao hutoa ushauri kwa wanaoanzisha vyama kuwa watawashauri vizuri kuhusu masuala muhimu na namna nzuri ya kuviendesha vyama hivyo ili vikubalike katika jamii.

Habari Kubwa