Uwezeshaji, uboreshaji  vituo afya uwe wa kasi

23Feb 2018
Mhariri
Nipashe
Uwezeshaji, uboreshaji  vituo afya uwe wa kasi

LICHA ya serikali kuendelea kuchukua hatua za kuwapatia wananchi huduma bora hususan katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu, bado zinahitajika jitihada za kuimarisha na kuboresha huduma hizo.

Hali hiyo inatokana na kero ambazo zimeendelea kuwakabili wananchi kutokana na baadhi kutozipata kabisa au huduma hizo kutowatosheleza wengine.

Malalamiko ya wananchi kuhusu kero za kukosa shule, vituo vya afya na zahanati, maji na barabara ni changamoto zinazotolewa kila siku katika maeneo yote nchini.

Hilo linadhihirika wazi wakati wa ziara za viongozi wanapofanya ziara na kukutana na wananchi hususan wa vijijini. Vile vile kero hizo zimekuwa zikitolewa na wananchi kupitia vyombo vya habari mara kwa mara.

Taarifa za wanavijiji kukosa kituo cha afya kwenye kata yao na kufuata huduma katika kata nyingine au wanakijiji kukosa zahanati na kufuata huduma za afya kijiji kingine ni habari ambazo zinajitokeza mara nyingi kwenye vyombo vya habari. Ubovu wa barabara na ukosefu wa majisafi na salama pia ni malalamiko ya kila uchao.

Kutokana na kilio cha wananchi kuhusu kero hizo na viongozi kuzipatia ufumbuzi ni jambo lisilo na ubishi kuwa serikali ya awamu ya tano imejielekeza zaidi katika kupunguza kero hizo kama si kuzimaliza kabisa.

Kwa mfano, Jumatatu wiki hii serikali ilisema kuwa kiasi cha Sh. bilioni 2.6 zimepelekwa katika Jiji la Mwanza kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa vituo vya afya.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile, wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akikagua na kuweka jiwe la msingi la kituo cha afya cha Karume wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, uboreshaji huo ulihusisha ujenzi wa chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na uboreshaji wa kituo hicho, ambapo serikali inatarajia kupeleka Sh. milioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi. Uboreshaji wa kituo cha afya cha Karume umegharimu takriban Sh. milioni 497 hadi sasa.

Awali, Waziri Mkuu alifungua zahanati ya Bulale iliyopo katika Kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana na kisha alitoa vitambulisho vya matibabu kwa wazee 250. Jumla ya wazee 5,398 wilayani humo wamepatiwa vitambulisho vya matibabu.

Hatua ya serikali kupeleka fedha kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya afya ni ya kupongeza kwa sababu inaenda sambamba na jitihada za kuimarisha na kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ambazo ni changamoto kwa wengi.

Ikumbukwe kuwa malalamiko juu ya huduma muhimu za kijamii ikiwamo afya yanatokana na kumgusa kila mwananchi wakati uwezo wa serikali kugharamia huduma hizo ni mdogo.

Kutokana na umuhimu huo, tunatoa rai kwa serikali kuendelea na jitihada za ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya, ili baadaye lengo la kila kata kuwa na kituo cha afya sambamba na kuwa na mahitaji yote muhimu vikiwamo vifaa tiba.

Kutokana na serikali kuendelea kuongeza bajeti ya sekta ya afya kila mwaka, mbali na kuboresha huduma za afya, pia ni matumaini yetu kwamba hatua hiyo itawezesha kufikiwa kwa lengo la serikali la kila kijiji nchini kuwa na zahanati.

Afya za wananchi ni muhimu kwa kuwa kinyume chake, ujenzi wa taifa hauwezi kuwa wa tija wala ufanisi. Mbali na kuongeza bajeti ya afya, jambo lingine muhimu ni usimamizi makini na wa karibu wa fedha zinazoelekezwa katika sekta hiyo. 

 

Habari Kubwa