Umakini utawale Kamati ya almasi

07Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Umakini utawale Kamati ya almasi

KATIKA mwendelezo wa jitihada za kusimamia rasilimali za nchi kuhakikisha kuwa zinawanufaisha Watanzania, Bunge limeunda Kamati Maalum ya ushauri kuhusu mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi.

Kamati hiyo iliundwa juzi ambayo ilikuwa siku ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Kamati hiyo itakuwa na wajumbe tisa watakaoongozwa na Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu,  na itafanya kazi kwa siku 30 kuanzia Julai 10, mwaka huu.

Ndugai alisema ameunda kamati hiyo kupitia Waraka wa Spika namba 3 wa mwaka huu na kuwataja Wajumbe wengine ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Dk. Immaculate Sware Semesi; Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Shally Raymond; Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF); Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula (CCM); Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Restituta Mbogo na Mbunge wa Wawi, Ahmed Juma Ngwali (CUF); Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) na Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM).

Kamati hiyo itatathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini kisha kuandaa mapendekezo mahsusi kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya madini hayo nchini.

Tunampongeza Ndugai kwa kutekeleza ushauri aliopewa na Rais John Magufuli Juni 12, mwaka huu alipohudhuria mkutano wa Rais wa kupokea taarifa ya Kamati ya Pili ya Masuala ya Kiuchumi na Kisheria kuhusu Usafirishaji wa Makinikia ya dhahabu ambapo Rais alipendekeza Bunge liunde Kamati ya kuchunguza na kufuatilia madini ya almasi.

Pia Ndugai anastahili pongeni kwa kuteua wajumbe wa kamati hiyo kwa kuzingatia vigezo alivyovitaja kuwa ni vya taaluma, uzoefu, pande za Muungano, jinsia na uwakilishi wa vyama vya siasa bungeni.

Uzingatiaji wa vigezo hivyo unatoa taswira kuwa ni kamati yenye uwakilishi na pia yenye watu wenye weledi wa kutafuta ukweli kuhusu uchimbaji wa madini hayo na kutoa ushauri wenye tija kwa serikali katika usimamizi wa madini hayo muhimu.

Ni kwa sababu hiyo tunajenga matumaini kwa wajumbe aliowateua Ndugai kuwa watatekeleza majukumu yao kwa kuchapa kazi na kutanguliza uzalendo, uadilifu, uaminifu na weledi kwa muda wote wa siku 30 kuanzia Jumatatu ijayo ambazo Kamati hiyo itafanya kazi katika ofisi za Bunge mjini Dodoma.

Tunashauri kwamba ili kupata taarifa za kutosha, itakuwa vizuri kama Kamati itapata siku kadhaa za kwenda katika nchi kadhaa ambazo zimefanikiwa kunufaika na almasi ili kupata uzoefu wa mbimu zilizotumika kusimamia rasilimali hiyo.

Tunafahamu kuwa kuna changamoto ya muda na bajeti, kama alivyosema Ndugai, lakini safari ya nje itakuwa na manufaa makubwa kwa kuwa itasaidia sana kamati katika kutoa mapendekezo mazuri na yenye tija kwa serikali.

Suala lingine la kuzingatia ni kwamba serikali iijengee Kamati mazingira bora ukiwamo ulinzi kama ilivyofanya kwa kamati zilizochunguza makinikia ya dhahabu kuepusha usumbufu kutoka kwa watu wenye maslahi na wanaonufaishwa na almasi.

Ili kutekeleza jukumu walilopewa wajumbe kwa tija na ufanisi, hawanabudi kuwa makini kama walivyofanya wajumbe wa kamati mbili za makinikia ya dhahabu, hivyo kuibua ukweli na kujipatia sifa kutoka kwa Watanzania na Rais Magufuli aliyeziunda.

Umakini ndio utakaowawezesha kufanyia kazi hadidu zote walizopewa na kuja na majibu kuhusu changamoto zilizopo katika madini ya almasi na kupendekeza hatua za kuchukua.

Habari Kubwa