Tunataka uchaguzi huru na haki TFF

17Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Tunataka uchaguzi huru na haki TFF

MCHAKATO wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) umeanza rasmi jana ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania uongozi.

Kwa siku ya kwanza tu ya kutolewa fomu hizo zaidi ya wadau 15 wa soka wamejitokeza kuchukua fomu tayari kuwania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 12 mkoani Dodoma.

Hii ni haki ya kikatiba ya TFF kwa wadau wa soka wenye sifa kujitokeza kuwania uongozi kwenye uchaguzi huo ambao viongozi wake watakaopatikana watakaa madarakani kwa miaka mitano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine.

Kama zilivyo chaguzi nyingine za kawaida, mambo mengi yanatokea katika kipindi cha mchakato wa uchaguzi mpaka kufikia siku yenyewe ya uchaguzi kwa kuwa kila mmoja anawania nafasi ya kungia kwenye uchaguzi wa soka ndani ya TFF.

Matukio ambayo mara kwa mara yamekuwa yakilalamikiwa wakati wa mchakato na mpaka kufikia siku ya uchaguzi ni pamoja na rushwa, kampeni chafu pamoja na hila mbalimbali za uchaguzi kutoka kwa wagombea, wapiga kura na hata kwa wadau mbalimbali wa soka.

Nipashe tunawakumbusha Kamati ya uchaguzi wa TFF, wagombea pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu ambao watapiga kura kuchagua viongozi, tunataka kuona uchaguzi wa huru na haki.

Tunaamini viongozi watakaochaguliwa kuongoza Shirikisho hili watakuwa wamepata kura nyingi miongoni mwa wagombea wote katika uchaguzi huu.

Hivyo ni vizuri yule atakayeshinda apewe nafasi yake ya ushindi na pasiwe na figisu figisu kwa kuwa Watanzania na wadau wa soka hawataki kuangalia jina la mtu, ila wanataka kiongozi atakayekuwa na mapenzi na soka letu na yule ambaye atakuwa na uwezo wa kuleta maendeleo kwenye soka letu.

Lakini pia kabla ya siku ya uchaguzi, kuna takribani siku tano za kwa wagomea kufanya kampeni wakinadi sera na mipango yao ili kujaribu kuwashawishi wajumbe wawapigie kura.

Hapa napo kuna tatizo kwa sababu baadhi ya wagombea wanatumia vibaya kampeni zao kwa kuwachafua wenzao kwa mambo mbalimbali yasiyokuwa ya ukweli ili tu kuhakikisha wanashindwa kwenye uchaguzi.

Nipashe tunaiomba Kamati ya Uchaguzi kuhakikisha kila kitu kinafanyika katika maadili yanayokubalika na kanuni za uchaguzi za TFF.

Muda utakapofika, hakuna haja ya kuwapo na kampeni za matusi kwa kuwa hiyo haitamjenga mgombea na haitashawishi wajumbe kuwapigia kura za kuwaweka madarakani.

Kwa wagombea wanapaswa kufahamu kuwa sera nzuri na mipango madhubuti na inayoweza kutekelezeka ndiyo itakayowaweka madarakani.

Tunahitaji kuona soka letu linapiga hatua kutoka hapa lilipo sasa na kusonga mbele zaidi, furaha ya Watanzania na wadau wa soka ni kutaka kuona licha tu mpira kuchezwa lakini pia mafanikio ya kimataifa.

Wajumbe ambao ndio wanabeba dhamana ya wadau wote wa soka ya kuchagua viongozi wetu wa soka, wanapaswa kuhakikisha wanachagua watu sahihi watakaotupa mafanikio.

Miaka mitano ni machache lakini ni mingi endapo tutakuwa na viongozi watakaolirudisha nyuma soka letu kwa kuwa itatupaswa kusubiri tena miaka mitano mingine ili kuwaondoa madarakani na hapo soka letu litakuwa limezidi kudidimia kama sio kufa kabisa.

Weredi na uchu wa mafanikio iwe msingi wa wajumbe wetu kuchagua watu sahihi kwa ajili ya soka letu.

Nipashe tunawatakia kila heri wale wote waliochukua fomu za kuwania uongozi na hata wale wanaoendelea kuchukua fomu, tunawatakia mchakato mwema wa uchaguzi.

Habari Kubwa