TAKUKURU inastahili pongezi, iungwe mkono mapambano dhidi ya rushwa

11Jun 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
TAKUKURU inastahili pongezi, iungwe mkono mapambano dhidi ya rushwa

KATIKA gazeti hili toleo la jana, habari iliyobeba uzito mkubwa ni ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuokoa takriban Sh. bilioni 54 ambazo wajanja wachache walitaka kuziiba kutoka katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Fedha hizo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati wa mkutano wa Chama cha Wabunge cha Kupambana na Rushwa Afrika (APNAC), ni miongoni mwa zile zilizotengwa kwenye bajeti ya kwanza ya uongozi wa Rais John Magufuli (mwaka 2016/17) ambayo utekelezaji wake unamalizika Juni 30, mwaka huu.

Aidha, katika taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri Mkuu kassim majaliwa alipokuwa akifungua mkutano huo, ilibainishwa kuwa taasisi ambazo zimeonekana vinara katika vitendo vya rushwa ni pamoja na mahakama, polisi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kuokolewa kwa kiasi kikubwa cha fedha hizo ambazo zingesababisha miradi mbalimbali ya maendeleo kukwama ni hatua kubwa na ya kujivunia na inadhihirisha kwamba Takukuru anafanya kazi nzuri katika mapambano dhidi ya rushwa.

Tunasema hivyo kwa sababu kiasi hicho ni kikubwa karibu mara tisa kulinganisha na Sh. bilioni saba zilizookolewa na taasisi hiyo katika mwaka wa fedha wa 2015/16.

Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba katika hotuba yake hiyo, Waziri Mkuu alisema mafanikio hayo yametokana na operesheni mbalimbali zinazofanywa na Takukuru nchini kote katika kuhakikisha wajanja wachache wanaoendelea kufuja fedha za umma wanadhibitiwa ipasavyo na wale wanaobainika kuchukuliwa hatua.

Aidha, mafanikio hayo yameonekana baada ya taasisi hiyo kuwezeshwa na kufanyiwa mabadiliko makubwa ya kiuongozi. Sambamba na hilo, hali hiyo inatokana na jitihada za serikali katika kupambana na rushwa na ufisadi kama Rais magufuli alivyoahidi wakati akiingia madarakani.

Kutokana na ahadi hiyo, kumekuwa na hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa katika wizara na taasisi mbalimbali za serikali zikiwamo zile nyeti kama bandari na polisi vigogo mbalimbali kuondolewa na moja ya sababu ikiwa kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya taasisi hizo za umma.

Kwa mafanikio hayo, Takukuru inastahili pongezi kutoka kwa kila Mtanzania mwenye mapenzi na nchi hii. Aidha, hatua hiyo inatokana na utashi wa uongozi na uthubutu katika kutenda.

Fedha hizo kama zingeingia mifukoni mwa wajanja hao, ni dhahiri kwamba wananchi wangekosa huduma muhimu. Tunasema hivyo kwa sababu kama kiasi hicho kingeelekezwa katika miradi ya maji, wananchi wengi wangeondokana na adha ya kufuata huduma hiyo umbali mrefu na matokeo yake wangetumia muda wa kuchota maji kuzalisha mali na hatimaye kuondokana na umaskini.

Pamoja na mafanikio hayo yaliyowezesha kuokoa mabilioni ya fedha yaliyokuwa yaingie katika mifuko ya wajanja wachache, wasio na uso wa aibu licha ya serikali kuweka wazi kwamba haina msalie mtume na wabadhirifu na wala rushwa, jitihada zaidi zinatakiwa kufanywa ili kutokomeza vitendo hivyo ambavyo si tu vinanyima watu kupata haki, bali ni adui wa maendeleo.

Kwa mantiki hiyo Watanzania wote wanapaswa kuungana na Takukutu na serikali kwa ujumla kuhakikisha vita dhidi ya rushwa vinakuwa na mafanikio kwa kuwafichua wale wote wanaojihusisha na wizi, ubadhirifu na udanganyifu katika matumizi ya fedha za umma.

Habari Kubwa