Stars msiidharau Lesotho leo

10Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Stars msiidharau Lesotho leo

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' leo inashuka kwenye Uwanja wa Taifa kucheza mchezo wa kwanza kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Afrika (AFCON) za mwaka 2019.

Stars inacheza na Lesotho hapa jijini Dar es Salaam mchezo ambao Watanzania wengi watataka kuona Stars inapata ushindi.

Inawezekana Watanzania wengi na wafuatiliaji wa soka wakaipa nafasi kubwa Tanzania kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo, lakini Nipashe tunawakumbusha wachezaji wa Stars na benchi la ufundi kwa ujumla kutowadharau wapinzani wao hao kama kweli wanahitaji ushindi.

Kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la soka Duniani (FIFA), Tanzania ipo nafasi moja juu dhidi ya wapinzani wao wa leo, Lesotho.

Tanzania imeporomoka kwa nafasi nne kutoka nafasi ya 135 mpaka nafasi ya 139 huku Lesotho yenyewe ikipanda kwa nafasi tisa kushika nafasi ya 140.

Kuwa juu ya Lesotho haina maana kuwa Tanzania imeizidi sana Lesotho, wachezaji na benchi la ufundi la Stars wanapaswa kuchukua tahadhari kwenye mchezo wa leo kwa kuwa lolote linaweza likatokea.

Tunaamini Stars imepata maandalizi ya kutosha na ikumbukwe juzi imewasili nchini ikitokea Misri ilipokwenda kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa leo.

Wadau wa soka na Watanzania kwa ujumla wanategemea ushindi kwenye mchezo wa leo hivyo ni jukumu la wachezaji kupambana kuhakikisha Tanzania inafanya kweli kwenye mchezo wa leo.

Wachezaji wanapaswa kukumbuka ushindi kwenye mchezo wa leo sio tu utaipa Stars mwanzo mzuri kwenye kundi lake, lakini pia watajiongezea pointi kwenye viwango vya soka vinavyotolewa na FIFA.

Hatutegemei visingizio kama tutashindwa kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo, Nipashe tunawaomba wachezaji kuingia uwanjani kupambana kwa ajili ya Taifa lao.

Tunafahamu mchezo wa leo watakuwepo nyota wa Tanzania wanaocheza soka nje ya nchi, Mbwana Samatta, Farid Mussa na Thomas Ulimwengu.

Ni vyema basi wachezaji wote wakaunganisha nguvu zao na kusiwe na utegemezi kutoka kwa nyota hawa kwa kuwa peke yao hawawezi kuipa ushindi Tanzania.

Nipashe tunaitakia kila la heri TaifaStars na Watanzania wote tutakuwa nyuma yao tukiamini ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo.

Ushindi kwenye mchezo wa leo utaipa mwanzo mzuri Taifa Stars kwa kuwa bado watakuwa na michezo mingine kwenye kundi lao.

Ikumbukwe Stars imepangwa kwenye kundi L ikiwa na timu nyingine za Uganda, Cape Verde pamoja na wapinzani wao wa leo, Lesotho.

Wakati Stars wakiumana na Lesotho, majirani zetu Uganda wenyewe wanaonyeshana kazi za Cape Verde na timu yoyoteitakayoshinda mchezo wake itakuwa imeanza vizuri harakati za kusaka tiketi kuelekea kwenye fainali hizo za Afrika.

Kama Stars itapambana na kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mechi zake hasa za nyumbani itakuwa imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kushiriki fainali hizo za Afrika kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 37.

Habari Kubwa