Sheria zifuatwe kudai haki, polisi pia itumie busara

18Jun 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Sheria zifuatwe kudai haki, polisi pia itumie busara

MIONGONI mwa matukio yaliyovuta hisia za wengi katika jiji la Dar es Salaam ni mapambano kati ya watu wenye ulemavu ambao ni madereva wa pikipiki za magurudumu matatu maarufu kama Bajaj na askari polisi.

Hatua hiyo ilitokana na walemavu hao waliokuwa wamekusanyika na kufunga barabara ya Sokoine kwa lengo la kwenda katika ofisi ya Mkurugenzi wa manispaa ya Ilala kulalamikia kile walichodai kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani wakati wanaendesha bajaj zao hizo.

Kufungwa kwa barabara hiyo kulisababisha usumbufu kwa wananchi wanaotumia ama kwa miguu au kwa kuendesha na kusafiria vyombo vya moto, hivyo kuwafanya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji hao.

Kutokana na hali hiyo, polisi katika taarifa yao walisema waliwakamata watu 40 akiwamo mwanamke mmoja kwa madai kwamba watu hao walifanya mikusanyiko isiyo na kibali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Ni ukweli kwamba watu hao walikuwa na haki ya kukusanyika na kuandamana kama katiba ya nchi inavyoelekeza lakini walichokosea ni kutokuwa na ruhusa ya kufanya hivyo.

Kwa ujumla zipo sheria na kanuni zinazoelekeza ni namna gani watu wanaweza kukusanyika na hata kufanya maandamano ya amani ili kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa kwa walengwa.

Pamoja na ukweli huo, walemavu hao walikosea kwa kushindwa kufuata taratibu kama zinavyoelekeza ndiyo maana hata walipojaribu kufanya hivyo, walikumbana na mkono wa dola baada ya kupigwa mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya na hata wengine kuishia mikononi mwa polisi.

Inawezekana kuna ukweli kwamba walemavu hao ambao baadhi yao huendesha bajaj kwa ajili ya kubeba abiria na kuiongezea kipato wamekuwa wakinyanyaswa na polisi hasa wale wa usalama barabarani kwa kukamatwa mara kwa mara.

Hata hivyo, njia walioyoitumia katika kudai haki zao au kuwasilisha malalamiko kunakohusika haikufuata utaratibu. Kwa mantiki hiyo, kuwa mlemavu si ruhusa kufanya maandamano kwa kuwa sheria haibagui mtu kwa misingi ya hali, jinsia au hali yoyote ile.

Kwa maneno mengine, walemavu hao, pamoja na kuwa nahaki ya kukusanyika, walipaswa hata kuchaguana kwa uwakilishi ili kufikisha malalamiko yao ili kuepusha athari kama zilizojitokeza juzi.

Pamoja na hayo, polisi nao hawakupaswa kutumia nguvu kiasi hicho dhidi ya walemavu hao kwa kuwa ni kundi la watu ambao wanaweza kuchukuliwa hatua nyingine bila kupigwa mabomu ya machozi kama ilivyofanyika.

Mara nyingi tumeshuhudia polisi ambao kazi yao kubwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao, wakitumia nafasi yao isivyostahili kwa kuwanyanyasa raia badala ya kuwalinda, kama kaulimbiu yao inavyobainisha.

Kwa msingi huo, ni vyema jeshi la polisi kabla ya kutekeleza majukumu yake likafanya tathmini yakinifu juu ya utelekezaji huo bila kuleta madhara kwa raia. Si kila sehemu wanapaswa kutumia nguvu kama ilivyofanyika kwa walemavu hao.

Ni vyema polisi wanapotekeleza majukumu yao kama vile kukamata wahalifu, wakatumia busara na kwa kuangalia manzigira ambayo wanafanya kazi husika badala ya kutumia nguvu za ziada ikiwamo kuwapiga raia mabomu.

Habari Kubwa