Serikali izingatie ushauri kuhusu mikopo ya ndani

14Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Serikali izingatie ushauri kuhusu mikopo ya ndani

SERIKALI imetahadharishwa kuwa makini kuhusiana na kukopa ndani ili kuepusha uwezekano wa kudhoofisha uchumi.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Kamati ya Bunge ya Bajeti, ikieleza serikali kwamba mikopo inayochukua kwenye taasisi za  ndani inaweza kudhoofisha ukuaji wa sekta binafsi kama serikali haitakuwa makini na hilo.

Maoni ya kamati hiyo yalisomwa juzi bungeni na Mwenyekiti wake, Hawa Ghasia, alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018.

Alisema Kamati imeona kuwa serikali imeanza kuwa na utaratibu wa kukopa zaidi katika vyanzo vya ndani, jambo ambalo katika uchumi haliwezi kuwa jema kwa kuwa taasisi za fedha zitakimbilia kuikopesha serikali kuliko sekta binafsi.

Ghasia alisema Kamati yake ina maoni kuwa iwapo utaratibu huo utaachwa uendelee utadhoofisha kwa kiwango kikubwa ukuaji wa sekta binafsi nchini.

Alisema hadi kufika Aprili 2017 serikali ilikuwa imekopa kiasi cha Sh. trilioni 4.7 sawa na asilimia 87.7 ya Sh. trilioni 5.37 zilizokuwa zimetarajiwa kukopwa kwa mwaka.

Tahadhari ya Kamati ya Bajeti ni ya msingi kwa kuwa utaratibu wa serikali kukopa katika taasisi za ndani hususani benki ni dhahiri kwamba kunatengeneza mazingira ya baadaye ya kuidhoofisha sekta binafsi.

Serikali inapokopa ndani, hali hiyo inaiweka sekta binafsi katika wakati mgumu kwa kuwa inakuwa vigumu kushindana na serikali kukopa katika taasisi za ndani.

Hali hiyo inatokana na serikali kuaminika kwa taasisi za fedha kwa kuwa ina dhamana ya uhakika katika kurejesha mikopo iliyokopa kama hati fungani na dhamana.

Uchumi wa nchi utakwenda vizuri ikiwa serikali itaachana na kukopa katika taasisi za ndani badala yake ikope nje kama kuna ulazima kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege.

Tunaamini kuwa kwa kufanya hivyo, kutatoa fursa kwa sekta binafsi kukua kwa sababu itakuwa na wigo mpana wa kukopa fedha kutoka katika taasisi za ndani.

Ikumbukwe kuwa sekta binafsi ina umuhimu mkubwa kwa kuwa ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, kwa kutilia maanani kuwa ndiyo inayoongoza katika uzalishaji wa bidhaa na kutoa ajira nyingi kwa wananchi kuliko serikali.

Kwa lugha nyingine, tunaweza kusema kwamba sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa nchi na hali hiyo itaendelea kuwa hivyo ikiwa serikali itaiwezesha kwa kuijengea mazingira mazuri kama fursa ya kupata mikopo ya uhakika na isiyo na masharti magumu kutoka kwenye taasisi za ndani, ikiwamo riba kubwa.

Riba kubwa inayotozwa na benki zetu hususani za binafsi imekuwa ikilalamikiwa kuwa ikaikwaza sekta binafsi na kupendekeza ipunguzwe na ikiwezekana iwekewe masharti na kufuatiliwa.

Baadhi ya benki binafsi hususani za kigeni zimekuwa zikilalamikiwa kupandisha ovyo riba bila utaratibu, hali inayosababisha wakopaji kujikuta wakidaiwa fedha nyingi baada ya kukopa na matokeo yake ni kunyang’anywa mali zao walizoweka kama dhamana kama ardhi, majengo na nyingine.

Mara kadhaa serikali imekuwa ikizitaka taasisi za fedha hususani mabenki kupunguza riba, lakini mwitikio haijaonekana, hivyo tunaishauri serikali kuingilia kati suala hilo ikiwa ni hatua nzuri na wezeshi kwa sekta binafsi kuendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu katika mazingira tulivu.

Ni matumaini yetu kuwa serikali itakuwa sikivu na kuachana na ukopaji katika taasisi za ndani.

Habari Kubwa