Klabu ziache mbwembwe kwenye usajili 2017/18

19Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Klabu ziache mbwembwe kwenye usajili 2017/18

KIPINDI cha usajili katika ligi mbalimbali za soka duniani kimeanza, huku nchini fujo za usajili zikiwa zimeanza kupamba moto.

Klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara zimeanza kusajili wachezaji kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao kueleka kwenye msimu mpya wa ligi Kuu utakaoanza Agosti.

Hiki ni kipindi ambacho masikio ya wadau wote wa soka yatasikia mengi juu ya wachezaji na klabu zetu zitakavyojiingiza kwenye usajili.

Tunaamini kipindi hiki kinapaswa kiwe cha makocha wa klabu zetu kuangalia namna ya kuboresha vikosi vyao kuelekea kwenye msimu mpya wa ligi.

Tunachokiamini ni kuwa makocha na mabenchi ya ufundi ndio wanaopaswa kufanya usajili kwa kuwa wao ndio wataalamu wa soka wanaojua kasoro walizobaini katika msimu uliopita 2016/17 na namna ya kuzitafutia ufumbuzi.

Makocha ndio wanaofahamu nafasi gani inahitaji mchezaji wa aina gani, hivyo kwa kifupi ndivyo inavyopaswa kuwa na sio vinginevyo.

Ndiyo maana ligi inapomalizika makocha wanakuwa na jukumu la kuandaa ripoti na kuiwasilisha kwa uongozi. Ripoti hiyo ndiyo inayokuwa na mapendekezo, yakiwamo ya wachezaji wapya, wanaotakiwa kubaki na wa kuacha.

Inapotokea viongozi wakafanya kazi ya kusajili wachezaji, wanapaswa kufanya hivyo kwa kufuata maoni na mapendekezo ya makocha wao.

Tanzania pengine ndio sehemu pekee ambapo viongozi wa klabu ambao wanapaswa kufanya mambo ya utawala, lakini wanaingilia jukumu la makocha la kusaka wachezaji na kuwasajili.

Kibaya viongozi hao wamekuwa wakisajili wachezaji kiushabiki pasipo kufuata mahitaji sahihi ya vikosi vyao na kujikuta wanapoteza fedha kwa kusajili wachezaji wasiowatumia.

Viongozi wa v ilabu vya Simba na Yanga vimekuwa mstari wa mbele katika hili kwa kusajili wachezaji kwa kukomoana na kujikuta baadhi yao wakiingia mkenge kwa kusajili wachezaji ambao hawahitajiki kwenye timu na hawamo katika mipango ya makocha.

Kwa mfano katika usajili wa msimu uliopita, Simba iliwasajili Peter Mwalyanzi kutoka Mbeya City ambaye pia alikuwa akiwaniwa na Yanga pamoja na Deus Kaseke, Simba ilimsajili pengine kwa lengo la kuikomoa Yanga, lakini wakajikuta wanamtoa kwa mkopo kwenye klabu nyingine baada ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Hivyo hivyo Yanga nayo ilifanya mchezo huo kwa kumsajili kwa mbwembwe mshambuliaji Matheo Anthony kutoka Zanzibar na kupewa jezi namba 10, lakini mpaka msimu umemalizika hakupata nafasi kubwa ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.

Ipo orodha ndefu wa wachezaji wa aina hiyo, hivyo tunavishauri vilabu vya ligi kuu kusajili wachezaji ambao watakuwa na mchango mkubwa kwenye vikosi vyao kwa ajili ya kuleta ushindani kwenye ligi.

Hiki ni kipindi kizuri kwa maandalizi ya timu kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu, maandalizi haya ni ya nje ya uwanja tukimaanisha usajili wa wachezaji.

Tungependa kuona ligi yetu inakuwa yenye ushindani mkubwa na ushindani huo unaweza ukawapo kwa kuwa na wachezaji wanaohitajika na wenye viwango kwenye timu zetu.

Viongozi wa vilabu waache usajili wa mbwembwe, badala yake usajili ufanyike kwa kufuata maoni na ushauri wa mabenchi ya ufundi ambalo kwa muda wote wa ligi wameona mapungufu ya timu zao na kujua ni aina gani ya wachezaji wanapaswa kuongezwa kwenye timu zao.

Usajili wenye tija ndio utakaozisaidia klabu zetu kufanya vizuri katika mechi za kimataifa. Wadau wa sokawanataka kuona ligi yenye bora na yenye ushindani zaidi msimu ujao, hivyo vikosi vya timu shiriki viimarishwe kwa usajili wenye tija kwa klabu.

Habari Kubwa