Msiba ni wa taifa tuomboleze,kutafakari

14May 2017
Ibrahim Mkamba
Nipashe Jumapili
Msiba ni wa taifa tuomboleze,kutafakari

TANGU wiki iliyopita, taifa liko kwenye msiba mzito baada ya kuondokewa na raia wake 35 ambao ni wanafunzi wa darasa la saba 32 , walimu wao wawili na dereva mmoja wote wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha.

Wapendwa hawa walifariki kwa ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu, mkoani Arusha. Unapozungumzia wanafunzi wa darasa la saba maana yake ni watoto wadogo waliozaliwa kuanzia mwaka 2004 tena hapo ni kurudi nyuma . Ni wasomi wachanga tena wadogo sana waliopoteza maisha mapema mno. Inauma sana kwa kweli, inasikitisha.

Inaumiza sana kwa Watanzania wengi kupoteza maisha kwenye tukio moja. Inatugusa zaidi kwani wengi wa Watanzania hao ni watoto wetu wakiwa wa umri wa miaka 12 mpaka 13. Inasikitisha sana kuwapoteza wataalam wawili ambao ni walimu, na inaumiza mno kumpoteza dereva, wote kutoka kwenye kituo kimoja cha kazi baada ya kupata ajali.

Ni wazi ndugu na jamaa zao wameumia mno kwani kuna watu waliokuwa wanawategemea dereva na walimu kwa ajili ya kuendesha maisha na pia wapo waliozifahamu ndoto za watoto waliopotea ambazo hawakuzisogelea, ukiachilia mbali kuzifikia.

Ni uchungu usiolinganishwa na chochote kingine. Pole nyingi kwa ndugu, jamaa na marafiki na kwa Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa wa kitaifa. Tumuombe Mwenyezi Mungu awapokee marehemu wote na kuwalaza mahali pema peponi.

Tuomboleze kwa kusimama kuwaombea wenzetu kabla ya shughuli zozote rasmi ikiwamo michezo na mikutano, sherehe na maadhimisho. Tukiendelea kuomboleza tunapaswa tujikumbushe mambo mawili makubwa, kwanza, kuchukua tahadhari kubwa tunapofanya jambo ambalo likiharibika linaweza kusababisha madhara makubwa au hasara kubwa kwa taifa.

Yaani kiwango cha uangalifu kiwiane na ukubwa wa hasara inayotazamiwa. Kwa mfano, magari yanayosafirisha watu wengi lazima yakaguliwe mara zote kabla ya safari na yawe na mikanda kwenye viti na abiria wajifunge.

Iwe lazima kila abiria afunge mkanda safarini. Naamini kama kila mmoja kwenye gari lililopata ajali angefunga mkanda, madhara yasingekuwa makubwa kama yalivyokuwa. Ni vizuri abiria kwenye gari walingane na idadi ya nafasi za viti ili wote wafunge mikanda.

Huko barabarani, alama za barabarani kama za kona kali, utelezi, mtelemko mkali, madaraja pamoja na michoro ya kwenye barabara inayozuia kulipita gari la mbele yako izingatiwe kwa kiwango kikubwa zaidi na dereva wa gari la abiria wengi kwani akipuuza, ikitokea ajali, hasara itakuwa kubwa zaidi. Hapa isitafsiriwe kwamba ninajua chanzo cha ajali iliyotuliza hadi tone la mwisho la machozi. Hapana, natahadharisha tu.

Pili, tusivuruge mipango mizuri ya baadaye kwa sababu hatua ya utekelezaji mipango hiyo sasa imetupa hasara. Tunachopaswa kufanya ni kuchukua tahadhari ya utekelezaji wa jambo hilo kwa siku zijazo. Hapa nazungumzia utaratibu wa watoto kutembeleana na kufanya mitihani ya ujirani mwema pamoja.

Huu ni mpango mzuri sana kwani una faida zaidi ya moja kwani kuna kupima uwezo lakini pia kuna watoto kukutana na wenzao.

Si vizuri kuuacha mpango huo mzuri bali cha kufanya ni kuhakikisha usafiri wa kutembeleana kwa malengo hayo ufanywe kwa kuzingatia usalama kama kuzingatia yaliyoelezwa hapo juu na pia kuzingatia hali ya hewa kuhusisha na hali ya barabara.

Hakuna sababu ya kusafiri na mvua kubwa kwenye barabara yenye utelezi. Tusiache kutembeleana kwa kuogopa ajali kama ambavyo hatupaswi kupuuza kufundishana kwa nguvu lugha za kigeni kama Kiingereza kwa sababu tuna mkakati wa kukiinua Kiswahili! Hoja hapa ni kwamba tusitafute sababu ya kujiondoa kutekeleza jambo lenye tija. Poleni sana Watanzania wote.

Habari Kubwa