Madiwani wacharukia fedha zao walizotoa kufukuza ‘ng’ombe wavamizi

23Feb 2018
Yasmine Protace
Nipashe
Madiwani wacharukia fedha zao walizotoa kufukuza ‘ng’ombe wavamizi
  • DED awaambia alizikabidhi ofisi ya DC
  • Mwenyewe ajibu ‘ni jambo la kiutendaji’
  • Mkaguzi wa Fedha asema haki yao kudai

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, wamekuja juu katika dai kwamba, wamegundua pesa walizojinyima mwaka mzima, ili zitumike kuondoa mifugo iliyozagaa katika vijiji mbalimbali wilayani hapa, inayohisiwa haijatumika kwa kusudi lake.

Katika dai lao, madiwani wanasema wamejinyima bajeti ya mlo wao katika vikao vya Baraza la Madiwani Mkuranga, kutoka bajeti ya Baraza la Madiwani, ili ifanye kazi ya kuondoa mifugo.

 

Madiwani hao wamedai wamejinyima kutokula chakula wakati wa mikutano na pesa husika inakuwa kwa ajli ya mifugo ya ng’ombe hao waliokuwa wamezagaa ovyo vijijini wakikitaja ni kiasi cha shilingi milioni saba.

 

Adolf Kowelo, ni Diwani wa Kata ya Mwandege Mkuranga, anayedai kwamba kisa cha kundi kubwa la ng’ombe kuingia wilayani Mkuranga na kuathiri mengi, ikiwemo uzalishaji mashambani, kunaleta m msukumo wa kila hatua inayopaswa kuchukuliwa, kurejesha mambo katika uhalisia wake.

 

Anaeleza utaratibu uliofanyika ni kwamba waliomba katika kikao cha Baraza la Madiwani kwamba, fedha za bajeti ya chakula chao cha mchana mkutanoni kwa mwaka wa fedha uliopo ndani ya miaka 10.

 

“Inashangaza kuona pesa imetolewa, lakini mifugo bado haijatolewa,”anasema na kuongeza kwamba,

wanachokihitaji sasa ni maelezo ya hizo fedha zinavyohitajika kutumika.

 

Rashid Selungwi, Diwani wa Kata ya Mbezi – Mkuranga, anadai ‘wameshinda njaa mwaka mzima’ kuridhia kuondolewa mifugo, lakini anaeleza kushangazwa mpaka sasa kuna mifugo na kinachotakiwa ni maelezo yanayohusu uwapo wa mifugo, ilhali fedha zikiwa zimeshatolewa.

 

Diwani wa Kata ya Mkamba, Hassan Dunda, anahoji inakuwaje pesa inatolewa, halafu mifugo bado inaendelea kuwapo?

 

Msimamo wake ni kwamba, hakubaliani na kiwango cha fedha Shilingi milioni saba, kutoa mifugo ambayo bado ipo inaendelea kurandaranda, hali inayoweza kusababisha hata mkaguzi akija kukagua

wilaya inaweza kupata hati chafu.

 

Shabani Manda, Diwani wa Kata ya Tengelea Mkuranga, anasema kuwa kiasi cha shilingi milioni 10 zilitolewa kwa makubaliano ya madiwani, ili

wasile iondolewe mifugo.

 

Anasema mwaka mzima wamekuwa hawali katika kipindi cha Baraza la Madiwani, lakini kinachoshangaza ni kuonyesha imetumia fedha Shilingi milioni saba, kwa ajili ya kuondoa mifugo.

 

Manda anasema, hivi sasa dai lao ni maelezo ya matumizi ya fedha hizo, iwapo zitashindikana,

basi warudishiwe fedha zao.

 

“Fedha mnasema zimetumika, mbona mifugo bado ipo? Tunaomba mrejesho wa matumizi ya hizo fedha kama hakuna basi mturudishie fedha

zetu,’’anafafanua.

 

DED

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Injinia Mushamu Munde, anasema kuwa fedha hiyo ilichukuliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkuranga, kwa ajili ya ya kuondoa hiyo mifugo.

 

“Hiyo fedha inayoongelewa, Kamati ya Ulinzi na Usalama, ilisema fedha ikabidhiwe katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkuranga na mpaka sasa

hatujapata mrejesho,’’anasema.

 

Hata hivyo, Manda anasema kwamba hawakubalini na taarifa za matumizi ya fedha Shilingi milioni

saba za kuondoa mifugo, bila ya kuonyesha mchanganuo wa matumizi hayo mpaka sasa.

 

Anasema iwapo itafika siku saba hawajapewa mrejesho wa matumizi ya dai hilo la mifugo, wanaitaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkuranga kuzirejesha fedha hizo.

 

MKAGUZI WA NDANI

 

Mkaguzi wa Ndani wa Fedha, Wilaya ya Mkuranga, Faidha Kassim, anasema utaratibu wa sheria, nyaraka za matumizi yote kisheria zinapaswa kuwasilishwa, kwani madiwani hao wanaolalamika wana haki ya kujua kiasi hicho kilichotoka kuhusiana na fedha zinazomhusu.

 

“Kama pesa zimetumika, zinatakiwa nyaraka ziletwe kwa madiwani na ni haki yao kuona kitu kilivyotumika,’’anasema.

 

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filbeto Sanga, ambaye maelezo yanaelekezwa kwake, hakupo katika kikao hicho cha kiserikali Mkuranga.

 

Baadaye Nipashe ilichuka hatua ya kumtafuta Sanga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkuranga, baada ya kukosekana kwa njia ya simu kwa siku kadhaa na alipopatikana alijibu, alikuwa anaelekea katika ujenzi wa Shule ya Msingi Kiparanga Mpakani na kutaka

mwandishi kumafuta wakati mwingine.

 

Katika jitihada za mwandishi wa makala kumtafuta kwa wakati mwingine Jumapili iliyopita, alitaka atumiwe ujumbe wa simu, ambao alirejeshea majibu yaliyosomeka: “Nakushauri kwa jambo hilo ni la kiutendaji, nilidhani busara kwako ni kuanza kujifunza.”

 

 

Habari Kubwa