Kijana unajiandaaje kujiajiri?

23Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kijana unajiandaaje kujiajiri?

MOJA ya dhana potofu miongoni mwa vijana wengi ni kutafuta elimu kwa lengo la kuajiriwa. Pengine  hiyo inatokana na mfumo dhaifu wa elimu katika nchi zetu, haijengei mwanafunzi mazingira ya ‘kusoma ili kuelimika’ bali ‘kusoma ili kujibu maswali ya mitihani kwa ufasaha!’

Shughuli za ujasiriamali, ambazo zinatakiwa kuwa sehemu ya dira ya vijana kujiajiri. PICHA: MTANDAO.

Vijana wengi kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na hata vyuo vikuu, wamekuwa wakihaha kutafuta ajira serikalini mara baada ya kuhitimu masomo yao, badala ya kuitumia elimu waliyoipata kujiajiri wenyewe.

Ikumbukwe kuwa mfumo wetu wa elimu nchini unazalisha vijana wengi kila mwaka wanaoingia katika soko la ajira.

Wengi ni watu wanaotafuta kuajiriwa, huku wachache wanaochagua kujitosa katika shughuli za ujasiriamali wakikumbana na vikwazo vingi ikiwemo wazazi wasioamini katika ujasiriamali, ukosefu wa mitaji, mrundikano wa kodi na masoko yenye ushindani yasiyotoa fursa sawa kwa biashara zinazoanza kukua.

 Ni kwa mantiki hiyo, basi baadhi ya wadau wa elimu wameona umuhimu wa kufundisha elimu ya ujasiriamali kuanzia ngazi ya sekondari hadi vyuoni, lengo likiwa ni kuwaandaa vijana wa kike na wa kiume kuitumia elimu hiyo kujiajiri wenyewe badala  ya kubaki  wakitegemea tu ajira kutoka serikalini.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa Tanzania ni moja ya nchi sita katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa na utajiri mkubwa wa rasilimali zaidi ya nchi nyingine katika jumuiya hiyo, lakini pamoja na utajiri huu wa nchi bado sehemu kubwa ya watu ni masikini wanaoishi kwa kipato cha sh. 2,000 kwa siku huku vijana wengi wakiwa hawana ajira za uhakika.

Aidha, shughuli kuu za kiuchumi ambazo ni kilimo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji wa madini na biashara ndogondogo zimekuwa zikifanyika kwa kutumia zana duni na mazingira yasiyo rafiki.

Tanzania inasifika kuwa moja ya nchi zenye amani na utulivu  mazingira ambayo yanatoa fursa pana ya uwekezaji kiuchumi.

Je kijana uliyeko nyumbani na shuleni umejiandaaje?

 

Habari Kubwa