Fursa za uwekezaji zilizopo na hitaji la mjadala mpana

19May 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Fursa za uwekezaji zilizopo na hitaji la mjadala mpana

MWAKA 1898 Rais wa 25 wa Marekani, William McKinley alianzisha utaratibu ulioonekana mpya kwa jamii ya Kimarekani, uamuzi wa kufanya biashara na China ambalo kwa wakati huo lilionekana taifa lililotengwa. Utaratibu huo uliitwa sera ya kufungua milango, au kwa Kiingereza ‘Open Door Policy.’

Sera hiyo hadi sasa inatumika nchini humo, ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kukuza uchumi na kuitwa taifa lenye uchumi mkubwa ulimwenguni. Marekani kunaelezwa “hata mtu akipeleka njugu zitauzika kwa faida kubwa.”

Inaelezwa, kinachotakiwa ni kuwa na bidhaa zenye ubora na viwango vya hali ya juu, kwani huko mazingira ya kufanya biashara ya uhakika kwa kila mwekezaji.

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu Tanzania, Benjamin Mkapa, mwaka 2001 ikiwa imebaki miaka minne kabla kumaliza uongozi wake wa miaka 10, alianzisha mithili ya ‘Open Door Policy.’ Ililenga kufungua fursa kwa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Sera hii ilipewa majina mengi ikiwamo uwekezaji, utandawazi na ubinafsishaji. Hii ni baada ya serikali kuwa na utaratibu wa kumiliki njia kuu za uchumi huku ikiwa na mbinu ndogo za kufanya biashara.

Ili kuweka rekodi sahihi baada ya kufungua fursa za uwekezaji kwa wafanyabiashara, Mzee Mkapa aliamua kuanzisha baraza la kuwakutanisha wawekezaji na serikali kujadiliana changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.

Aliliita Baraza la Taifa la Biashara (TNBC-Tanzania National Business Council) kupitia Waraka Namba Moja, rais aliyoutia saini kwa mkono wake Septemba 12, 2001.

Malengo ya TNBC ni kushauri na kusikiliza kero za pande zote mbili: Sekta binafsi na sekta ya umma. Yaani, baraza linakuwa daraja katika pande hizo mbili.

Kila mwaka kunakuwapo mkutano wa kujadili changamoto wanazokumbana nazo sekta zote mbili; ya umma na serikali. Hadi mwaka huu imeshafanyika mikutano 10.

Mkutano wa mwisho ulifanyika Mei 6 mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa mikutano hii kiutaratibu anakuwa rais wa nchi aliye madarakani kwa wakati huo.

NAFASI YA TNBC

Imerejewa historia fupi ya TNBC, katika lengo la kuingia kwa kina kuhusu nafasi ya baraza hilo kiutendaji.

Ingawa baraza hilo limeanzishwa kwa utaratibu wa kufungua milango kwa wafanyabiashara na wawekezaji,lengo hilo zuri linakutana na kasoro ya kuwapo mazingira yanayowakwaza wawekezaji; aidha kwa makusudi au kwa kutoelewana misingi na mipaka ya sheria zilizowekwa na mamlaka.

Katika awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, TNBC katika mikutano yake mingi, ajenda kuu imekuwa ni kuweka mazingira bora ya biashara nchini.

Bado kuna ukakasi kwa pande zote mbili kutoaminiana na haijulikani ama ni wawekezaji wanaoinyonya serikali au serikali ndiyo inawanyonya wawekezaji.

Katika mkutano wa saba, Mwenyekiti Jakaya Kikwete, aliamua kuundwe kikosi kazi cha kusimamia kuwapo mazingira bora ya biashara katika ardhi ya Tanzania. Hata hivyo, hadi anaondoka madarakani inaonekana, suala hilo lilikuwa halijapatiwa ufumbuzi.

“Kuimarisha mazingira ya biashara ni suala muhimu katika mikakati ya kukuza uchumi kwa Watanzania wengi,” alitamka Mwenyekiti Kikwete, katika Mkutano wa Saba wa Baraza.

Wajumbe 40 wa baraza hilo ambao hutokana na wajumbe 20 kutoka sekta binafsi na 20 sekta ya umma, waliafikiana katika mkutano wa sita kuwa PDB kwa kushirikiana na TNBC na TPSF (Taasisi ya Sekta Binafsi), wasimamie masuala mtambuka yanayoonekana kujirudia kila mwaka katika malalamiko ya sekta binafsi.

Idara maalumu ndani ya ofisi ya Rais iitwayo PDB, ilianzishwa mwaka 2013, lengo ni kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Malalamiko hayo ni upatikanaji ardhi, mikopo nafuu ya benki, kodi, mikataba ya kimataifa na sheria ya kazi.

Kimsingi, masuala haya yameendelea kuwa kikwazo kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa kipindi kirefu hadi katika mkutano wa mwaka huu ulikua mjadala mkubwa katika maeneo hayo hasa mlolongo mrefu wa tozo na kutoshirikishwa katika mabadiliko ya sera na ulipaji kodi.

Hiyo yote inaangukia katika mazingira bora ya uwekezaji na ndiyo maana, Rais mstaafu Kikwete wakati wa mkutano wake wa mwisho kuwa mwenyekiti wa baraza alisema: “Tunahitajika kuweka mazingira bora ya biashara ikiwa tunataka kuimarisha maendeleo endelevu.

“Nakiri biashara ndiyo itakayoleta maendeleo nchini na hatimaye kufuta umasikini. Hili pia linanikumbusha kuwa, ili biashara iwe huru na nafasi ya kutosha hakuna budi taifa liweke mazingira bora ya wawekezaji na hii ni kazi ya serikali kufanya yote haya.

“Lazima serikali na sekta binafsi wawe na majadiliano murua yatakayoleta mabadiliko kwenye biashara na uwekezaji.”

Katika mkutano wake wa kwanza kuuongoza, Rais Dk. John Magufuli, aliweka wazi dhana hii iliyozungumzwa na mtangulizi wake, lazima serikali iwe karibu na sekta binafsi, ili kujua matatizo yao.

Wakati ratiba ya mkutano wa 10 ikisomwa, ilionekana mjadala kati ya sekta bianfsi na umma, ungechukua chini ya saa moja, takribani dakika 45 na saa nyingine zingetumika kwa hotuba na taarifa za serikali.

Mwenyekiti alisema, lazima sekta binafsi zipewe muda wa kuzungumzia dukuduku waliyo nayo, hivyo zilitumika saa tatu za kuwasikiliza wafanyabiashara wana nini na serikali ilipewa muda wa kujibu.

Malalamiko makubwa yalikuwa ni yale yale yanayojirudia kila mkutano: Mazingira bora ya biashara, mlolongo wa kodi na huduma duni zinazotolewa na mamlaka za serikali pamoja na ugumu wa upatikanaji ardhi.

Msingi wa makala haya ni kutaka kusisitiza umuhimu wa kuanzishwa TNBC; daraja la kuunganisha sekta binafsi na sekta ya umma. Sekta hizo mbili, zinahitaji mijadala ya mara kwa mara kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.

MUUNDO WA BARAZA

Wakati Rais ni Mwenyekiti wa Mikutano ya Baraza Ngazi ya Taifa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya, ni wenyeviti wa baraza katika maeneo yao ya uongozi.

Mkurugenzi wa Mazingira ya Biashara TNBC, Arthur Mtafya alishawahi kusema kuwa hali si shwari katika mazingira ya biashara na hasa mikoani, wananchi hawana elimu kuhusu umuhimu wa mikutano ya baraza.

“Ushirikishwaji wananchi ni jambo kubwa na hili hasa linafanyika kupitia mikutano inayoandaliwa na wakuu wa mikoa na wilaya. Kwa sababu, unaweza ukampa ardhi mwekezaji kumbe wakazi wa eneo hilo wana mpango wa matumizi tofauti, kama kuchunga mifugo, makaburi au sehemu ya michezo, hapo ndipo vurugu inapoanzia,” anasema Mtafya.

Kingine cha msingi, ni ushirikishwaji wananchi kiuchumi, Local Content hasa katika sekta ya madini na gesi. Serikali ya Awamu ya Nne, iliona umuhimu wa kutunga sera hii ya kuwapa fursa wananchi kushiriki kwenye shughuli za mafuta na gesi iliyotiwa saini Mei, 2015.

Hii ilikuwa ajenda namba mbili katika mkutano wa saba wa baraza, ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu ilipewa kazi ya kuunda kikosi kazi wakishirikisha TPSF na TNBC kueleza kwa wananchi maana ya ‘Local Content.’

Ieleweke kuwa, mafuta na gesi yanahitaji uwekezaji mkubwa, lakini serikali ikatafakari wananchi wa kipato cha chini watanufaika vipi na fursa hizi, ikaamuliwa shughuli ndogo ndogo kama udereva, ufundi na zabuni zinazohitaji mitaji midogo wapewe wazalendo kulingana na uwezo wao ili kila mmoja anufaike.

Kote huko tutafika ikiwa agizo au angalizo la Rais Magufuli kwa nafasi yake ya uenyekiti wa TNBC, litafuatwa pale aliposema kuwapo mikutano ya mara kwa mara itakayotoa fursa kwa sekta binafsi na sekta ya umma kujadiliana changamoto zilizopo kwenye mazingira ya biashara nchini.

Habari Kubwa