Zitto ajitwisha zigo la kodi

22Jan 2018
Joctan Ngelly
Nipashe
Zitto ajitwisha zigo la kodi

MBUNGE wa Jinbo la Kigoma Mjini ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amewataka wafanyabiashara wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki ambacho anafanya mchakato wa kupunguza kodi ya pango ya vibanda vya Manispaa.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) akihutubia wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwenye uwanja wa Mwanga Centre juzi, kuhusu kero ya ongezeko la tozo za vibanda katika soko la Mtambukwa. PICHA: MAGRETH MAGOSSO.

Vibanda hivyo vipo maeneo ya Mwanga na Kigoma Mjini na lengo lake ni kutaka kodi ipungue kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 30,000 ambayo ilikuwa imepitishwa na waziri mwenye dhamana.

 

Zitto aliyasema hayo, wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi, kwenye uwanja wa Mwanga Manispaa ya Kigoma/Ujiji na kufafanua kuwa fedha walizokuwa wakipata kwenye kodi ya majengo Serikali Kuu imezichukua.

 

“Tumefunga mwaka na sisi tumekusanya bilioni moja tu kwa sababu fedha nyingine zote zimekwenda Serikali Kuu, kwa hiyo ndugu zangu tuwe wavumilivu mambo yatakuwa sawa.”

 

Alisema baada ya kuwasikiliza wafanyabiashara hao maamuzi yake yalikuwa kubadilishwa kwa sheria ndogo kwa mujibu wa taratibu, ili tozo ya vibanda ipande kutosha Sh. 15,000 mpaka Sh. 30,000 badala ya kuwa Sh. 50,000 kwa mwezi katika  masoko ya Mwanga na Kigoma Mjini.

 

Aidha, Zitto ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji kufanya tathmini yote kwenye masoko, ili iweze kuwafidia wale ambao walijenga vibanda kwenye masoko hayo na iweze kuwalipa fidia, halafu wafanyabiashara wanaouza wapewe mikataba na Manispaa hiyo.

 

“Tunataka yule ambaye anabeba mzigo mkubwa tumpunguzie mzigo alipe tozo ya Manispaa peke yake na ushuru wa soko, tumuondolee tozo ambayo anamlipa aliyempangishia kibanda.

Hicho ndicho nilichokifanya, mimi siwezi kufanya vitu vinavyowaumiza wazazi wangu, dada zangu, wadogo zangu, kaka zangu na shangazi zagu.

 

“Haiwezekani nitakuwa mtu wa ajabu sana, kesi za namna hiyo tutazishughulikia ili tuwaondolee mfanyabiashara mzigo, ili abakie analipa tozo moja ya Manispaa peke yake kuliko kulipa tozo ya mwenye kibanda na Manispaa,” alisema.

 

Wakati huo huo, Zitto alisema kuwa Sh. bilioni 26 walizozipata kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya miradi ya ujenzi ya barabara za lami katika Halmashauri ya Manispaa hiyo, ujenzi wake utaanza Aprili 1 mwaka huu.

 

 “Nawaomba sana ndugu zangu tuwape ushirikiano makandarasi watakaokuwa wanafanya ujenzi wa barabara hizo za lami katika Halmashauri ya Manispaa yetu.”

 

 

 

 

 

Habari Kubwa