Waziri amtaka Kitwanga kutimka CCM

14May 2017
Sanula Athanas
Nipashe Jumapili
Waziri amtaka Kitwanga kutimka CCM
  • • Mwenyewe aja juu, aanika msimamo...

SIKU chache baada ya Charles Kitwanga kutishia kuzima mtambo wa kusukuma maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Shiyanga na Tabora, serikali imemjibu waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kumtaka ahame kwenye chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama anaona hatendewi haki.

Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji bungeni mjini hapa Jumatano, Kitwanga alitishia kuhamasisha zaidi ya wananchi 10,000 kwenda kuzima mtambo wa maji ulioko kwenye chanzo cha maji cha Iherere jimboni kwake Misungwi, mkoani Mwanza, ikiwa hawatapatiwa maji yatokanayo na mradi huo.

Hata hivyo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, akihitimisha mjadala wa makadirio hayo juzi. alimjibu mbunge huyo kwa kumtaka aihame CCM kama anaona hakitendi haki dhidi yake.

"Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la mchango wa Mheshimiwa Kitwanga. Amechangia hapa kwa hisia kubwa kuonyesha kuwa serikali ya CCM haijafanya chochote kwenye Wilaya ya Misungwi," alisema.

"Sasa nataka nimuulize Kitwanga kama yupo hapa kwamba hayo ni maneno yake au ya wananchi? Kama ni ya wananchi nitawaambia ni nini kimefanyika Misungwi kwani hata juzi tumetia saini mikataba ya maji na Mwenyekiti wa Halmashauri alikuwapo, ya kupeleka maji Misungwi kutoka Ziwa Victoria kwa fedha nyingi zaidi ya Sh. bilioni 38.

"Sasa anaposema anakwenda kuhamasisha wananchi wakabomoe mtambo wa Iherere, maana yake analeta uasi au hathamini kazi iliyofanywa na chama chake, sasa ajitoe kwenye chama kwa sababu serikali imepeleka fedha na maendeleo yaliyofanyika ni lazima tuwahamasishe wananchi kutunza miundombinu iliyopo badala ya kwenda kuibomoa.

"Hata kwenye umeme huwa tunaona wanaweka kwenye kijiji kimoja na kuruka hadi kijiji cha nne, lakini hatujawahi kuona wanang'oa nguzo. Sasa nataka nimwambie serikali inaendelea kuboresha maji katika maeneo mbalimbali ikiwamo Misungwi na Usagara."

Akizungumzia kuhusu Usagara, Waziri huyo alisema atapeleka maji yanayosumkumwa kutoka Nyashishi wakitarajia kuzalisha lita milioni tatu na usanifu unafanyika kwenye eneo la Buswelu.

Mhandisi Lwenge pia alisema Sh. bilioni 3.5 zitatumika katika mradi wa maji utakokwenda katika vijiji mbalimbali wilayani humo.
"Sasa akisema hauingi mkono, maana yake hizi fedha tuzitoe tupeleke wilaya nyingine," alisema.

"Mheshimiwa Naibu Spika, wizara yangu kupitia mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira, imesaini mkataba tayari wa Sh. bilioni 38 kwa ajili ya kupeleka maji Misungwi na kazi hiyo imefadhiliwa na Benki ya Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo la Ufaransa. Kwa hiyo, mtu wa Misungwi akisema hathamini kazi inayofanywa na serikali ni jambo linalosikitisha sana."

Katika mchango wake, Kitwanga alisema anashangaa kuona serikali inapeleka maji mikoa ya Shinyanga na Tabora kwa zaidi ya Sh. bilioni 600 huku wananchi wa vijiji vya Wilaya ya Misungwi unamopita mradi huo vikiachwa bila maji.

“Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu hakuna maji ya uhakika na tangu mwaka 2008 wananchi wamekuwa wakiyasubiri bila mafanikio," Kitwanga alisema.

“Kwa hiyo, nitakachokifanya safari hii, sitatoa shilingi kwenye bajeti, bali nitakwenda kuwahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000, twende tukazime mtambo katika kile chanzo cha maji ili wote tukose.

“Wanamchi wa Misungwi hawana maji na katika bajeti yenu leo (Jumatano) mmesema Nyang’omango kuna maji wakati hakuna, sasa nawaambia, sitatoa shilingi 'nita-mobilize' (nitahamasisha) wananchi tukazime ule mtambo.

“World Bank' (Benki ya Dunia) walifika pale kijijini, wakasema hawa wananchi walioko kwenye kile chanzo wanatakiwa kupata maji, lakini nyie hamuoni, hivi nyie mkoje?

“Nakipenda chama changu (CCM), nampenda Rais wangu (John) Magufuli, lakini lazima tutendeane haki kwa sababu hii nchi ni yetu sote.

“Hamuwezi kupeleka maji sehemu nyingine kwa gharama ya Sh. bilioni 600 halafu mkashindwa kuwapa wananchi wangu hata mradi wa Sh. bilioni 10.

“Mshukuru kwamba nilipokuwa waziri, nilikuwa siwezi kusema kitu, lakini sasa nimetoka, tutapambana kwa sababu lazima tuwe na mipango mizuri ya kuwapelekea wananchi wetu maji kama inavyofanyika katika umeme kupitia REA (Wakala wa Umeme Vijijini)."

Kitwanga pia alilalamikia kile alichokiita tabia ya baadhi ya viongozi wa wizara hiyo, kukwamisha upatikanaji wa maji kupitia kwa marafiki zake kutoka Austria.

“Rais alipokuja Misungwi, aliwaambia wananchi, kwamba nina marafiki zangu huko nje wanaoweza kunisaidia kupata maji," alisema. "Ule mradi ulipokuja, nikawekewa figisu wakasema mimi nina 'interest' (maslahi) nao.

"Ni kweli nina 'interest' nao kwa sababu wananchi wangu wa Kolomije wanahitaji maji, wananchi wa Bukumbi wanahitaji maji.

“Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena, safari hii sitatoa shilingi, nitakwenda kuwahamasisha wananchi wangu tukazime ule mtambo wa maji ili wote tukose,” alisisitiza Kitwanga.

'NIHAME CCM?'
Alipotafutwa na Nipashe jana nje ya Bunge kuzungumzia kauli hiyo ya Waziri Lwenge, Kitwanga alisema hafikirii kukihama chama hicho.

"Nihame CCM? Yeye (Waziri Lwenge) ndiye ahame. Mimi nimezaliwa CCM, nimekulia CCM na nitafia CCM," alisema Kitwanga.

Habari Kubwa