Walemavu 100 kutembea tena

22Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Walemavu 100 kutembea tena

ZAIDI ya watu 100 wenye ulemavu uliotokana na kupoteza miguu kwa ajali na magonjwa, watatembea tena baada ya kampuni ya Kamal Group kujitosa kuwasaidia kiungo hicho bandia. 

Kamali itasaidia walemavu hao kupitia mfuko wake wa Peoples’ Empowerment Foundation (PEF kwa kutoa miguu bandia kwa watu 108.

Bei ya mguu bandia mmoja katika hospitali za rufani nchini ni kati ya Sh. milioni moja hadi Sh. milioni tatu. “Sina la kuwalipa ila itoshe tu kusema ninashukuru sana kwa msaada huu," alisema Mwanaisha Mohammed ambaye "Sijaweza kutembea tangu nilipopoteza mguu wangu mmoja mwaka 2009. 

"Kwa sasa nitaweza kutembea na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda."

Image result for Walemavu 100 wapewa miguu na kampuni ya Kamal GroupAkizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa wahusika iliyohudhuriwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde, Mwenyekiti wa Kamal Group, Gagan Gupta alisema kampuni yake inaamini ina wajibu wa kusaidia maendeleo ya jamii inayoizunguka.

“Kamal Group inaamini ni wajibu wetu kuleta tabasamu katika nyuso za watu kuhakikisha wale wenye ulemavu wa miguu wanaweza kutembea tena na kusaidia katika kuijenga Tanzania yenye viwanda,” alisema Gupta.

Gupta pia alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa kusaidia kuwakusanya walemavu wa miguu wenye kuhitaji msaada huo.

Alisema ilianzisha mradi wa kutengeneza na kugawa bure miguu bandia miaka mitatu iliyopita na mpaka sasa kampuni yake inaendelea kufanya hivyo.

Naye Naibu Waziri Mavunde alisema kampuni hiyo imejidhihirisha ni rafiki wa kweli wa Watanzania na hatua kama hizo zinaifanya serikali kuzidi kufikiria jinsi ya kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara nchini. 

“Kama serikali, tutafurahi zaidi endapo kampuni nyingi zaidi zitaweza kuiga mfano huu na kwa kufanya hivyo, tutapata nguvu zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya biashara nchini,” alisema Mavunde.

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 3.6 wenye ulemavu. Kati yao, milioni 1.7 wanahitaji viungo bandia. Kuna Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 50. 

Takwimu za Chama cha Walemavu (Chawata) zinaonyesha ni asilimia 20 ya walemavu wa viungo ndiyo wenye uwezo wa kupata viungo bandia huku wengi wakilazimika kutembelea magongo.

Habari Kubwa