Polepole afichua siri CCM kushindwa Moshi

22Jan 2018
Godfrey Mushi
Nipashe
Polepole afichua siri CCM kushindwa Moshi

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) wa Itikadi na Uenezi,, Humphrey Polepole,-

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) wa Itikadi na Uenezi,, Humphrey Polepole.

Amefichua siri kuwa CCM kushindwa katika uchaguzi mkuu uliopita Jimbo la Moshi Mjini kulitokana na kudharauliwa kwa mabalozi wa nyumba kumi pamoja na kushindwa kuwa na taarifa sahihi za matatizo ya wananchi.

 

Jimbo la Moshi Mjini linaongozwa na upinzani tangu mwaka 1995. Mbunge wa sasa wa jimbo hilo ni Japhary Michael wa Chadema, aliyetwaa nafasi hiyo baada ya kustaafu siasa marehemu, Philemon Ndesamburo.

 

Polepole alitoa siri hiyo, wakati alipokutana na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Moshi Mjini pamoja na wanachama wakongwe wa chama hicho.

 

“Niwape siri sasa katika Jimbo la Moshi Mjini, CCM ilishindwa mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu uliopita kutokana na kuwadharau mabalozi, baadhi ya viongozi wa chama wamekuwa wakiwachukulia mabalozi kama watu wa chini,

 

Alisema: “CCM ya wakati huo ilishindwa kutambua taarifa sahihi za matatizo ya wananchi, sasa baada ya kutambua kosa hilo, CCM mpya sasa chini ya Mwenyekiti wake, Dk. John Magufuli, mabalozi wanapaswa kisikilizwa kwa sababu wao ndio kiungo baina ya chama na wananchi.”

 

Kwa mujibu wa Polepole, wapo baadhi ya viongozi wa chama hicho ni wa binafsi na huangalia maslahi yao kwanza na chama baadae.

 

Aliwataka viongozi kama hao waliopo Kilimanjaro wawapishe ili chama hicho kitekeleze wajibu wake wa kuwatumikia wananchi wote bila kujali vipato vyao.

 

Alisisitiza mara kadhaa, CCM imekuwa ikishindwa katika maeneo mbalimbali wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu kutokana na baadhi ya viongozi kutotimiza wajibu wao na kushindwa kuisimamia serikali.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, aliwataka wana chama wa chama hicho kuvunja makundi waliyoanzishwa kwa ajili ya kutafuta madaraka kwa kuwa uchaguzi umeshapita na viongozi wa kuongoza chama wameshapatikana, hivyo jukumu kubwa walilonalo ni kuwaunga mkono.

 

Habari Kubwa