Majaliwa 'atema  cheche' Butiama

22Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa 'atema  cheche' Butiama

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa , Mkewe Mary na Mama Maria Nyerere wakiwapungia wananchi katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika uwanja wa Mwenge kijijini Butiama. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema Halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotolewa na Serikali katika shughuli nyingine jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.

Pia Waziri Mkuu aliagiza kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama, Solomon Ngiliule pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri, Masanja Sabuni na Ofisa Manunuzi wa Halmashauri  hiyo, Robert Makendo.

Alisema viongozi hao wanatakiwa wachunguzwe kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwamo Sh. milioni 12 walizotumia kuandaa wasifu wa Halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu alisema fedha nyingine ni pamoja na Sh. milioni 70 za elimu maalumu na Sh. milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazijulikani zimetumikaje. 

“Hatuwezi kuvumilia vitendo hivi, fanyeni uchunguzi na naomba taarifa yake mara mtakapokamilisha," alisema Majaliwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) mkoani Mara imkamate na kumuhoji Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) mkoani Mara, Peter Salim  baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Butiama.

Waziri Mkuu alisema Serikali ilitoa Sh. milioni 600 Aprili, 2017 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya hiyo, lakini hadi sasa wakala huo haujafanya kazi yoyote.

Katika maelezo yake, Salim alisema ujenzi wa ofisi hiyo hadi kukamilika utagharimu Sh. bilioni tatu, na kwamba kati ya Sh. milioni 600 zilizotolewa na Serikali, Sh. milioni 400 zimetumika kujengea msingi, kauli ambayo ilipingwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Anna-Rose Nyamubi.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu siyo kweli kwamba kuna kazi inayoendelea bali kilichopo pale ni mashimo ambayo hayajulikani ni ya nini," alisema Nyamubi.

Waziri Mkuu baada ya kuwasili wilayani Butiama akiambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa walizuru kaburi la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, katika Kijiji cha Mwitongo na kufanya mazungumzo na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere.

Habari Kubwa