Waongoza utalii Zanzibar walia ‘papasi’ kuvamia biashara yao

23Feb 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Waongoza utalii Zanzibar walia ‘papasi’ kuvamia biashara yao
  • Kampuni rasmi ziko 230, zinazolipa kodi ni 30 tu
  • ‘Papasi ’ ni watu wanaofanya biashara ya kuongoza watalii Zanzibar kienyeji, yaani wasio na leseni za kufanya kazi hiyo watu ambao hawalipi kodi na wengi hawana hata ofisi za kufanya hayo wanayoyafanya.

SEKTA ya Utalii inaelezwa kuwa na mchango mkubwa sana kwa ukuaji wa uchumi Visiwani Zanzibar, kutokana na idadi kubwa ya watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wanaozidi kumiminika kujionea vivutio kadha wa kadha.

Pamoja na ukweli huo hivi sasa sekta hiyo imepata tishio kubwa la watu wanaojulikana kama ‘papasi ’ wanaoelezwa, iwapo hawatadhibitiwa basi wataiyumbisha na kudidimiza sekta hiyo nyeti kwa ukuaji wa uchumi.

‘Papasi’ ni watu wanaofanya biashara ya kuongoza watalii Zanzibar kienyeji, yaani wasio na leseni za kufanya kazi hiyo watu ambao hawalipi kodi na wengi hawana hata ofisi za kufanya hayo wanayoyafanya.

Jumuiya ya Chama cha Waongoza Watalii Zanzibar (ZATO), imeiona sasa hiyo ni hatari, hivyo imechukua hatua ya kuitahadharisha serikali kupitia Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kwamba iwapo watu hao watachekewa watakimbiza watalii kwani wengi hawana vibali na wanaikosesha serikali mapato.

Mwenyekiti wa ZATO, Hassan Ali Mzee, anatoa mfano akisema kazi hiyo hivi sasa inafanywa na kila mtu anayehisi kuwa anaweza kuifanya, hivyo kusababisha ifanywe kiholela yaaani bila kuzingatia maadili wala utaalamu wa kuwaongoza watalii, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa sekta hiyo muhimu.

“Hivi mtu akiwa na ‘kigari’ chake basi anaona anaweza kuongoza watalii, hawa watu hawana hata ofisi wala leseni za kufanyakazi hii lakini wanaokota watalii mitaani na kuwadanganya danganya kwamba watawatafutia hoteli za bei nafuu,” anasema na kuongeza:

“Ili mtalii arudi tena Zanzibar msimu mwingine, lazima avutiwe na safari yake. Sasa kama atakuja na kutapeliwa na hawa vijana, tunawaita ‘beach boys’ au ‘papasi’ hawezi kurudi tena na atawaambia wenzake kuwa kule si sehemu ya kwenda, ndiyo sababu tunaiomba Kamisheni ya Utalii Zanzibar iwaondoe kwenye biashara hii hawa watu,” anasema Hassan.

Kimsingi, ‘Beach boys’ ni vijana wa mitaani wasio na leseni au kampuni zilizosajiliwa kuongoza watalii wanaoshinda kudaka watalii katika maeneo ya fukwe na mitaani, kisha kuwahadaa kuwa wao wanaweza kuwatafutia vyumba vya bei nafuu.

Inadaiwa kwamba Zanzibar ina ‘papasi’ wanaopatikana hata kwenye taasisi na idara kadhaa za serikali, kwa maana kwamba watumishi wanashirikiana na watu hao wanafanya biashara kinyume cha sheria.

Hassan anaeleza, cha kushangaza ni kwamba kuna kampuni 234 Zanzibar zilizosajiliwa kwa ajili ya kuongoza watalii, lakini zinazolipa kodi serikalini ni 30 tu hivyo hizo zingine zinafanya kazi kwa kuiba, hivyo kuikosesha serikali mapato.

“Sasa unaweza kufikiria hapo kama wanaolipa kodi ni 30 tu kati ya 234. Ina maana wanachama wa ZATO wataishi vipi? Wanachama wa ZATO wanalipa kodi zote serikalini watashindanaje na hawa watu ambao hawalipi kodi?’ anahoji.

Anasema chama chao kimekuja na mapendekezo ambayo watayawasilisha serikalini hivi karibuni, wakitaka kupewa jukumu pia la kupitia wasifu wa watu wanaoomba leseni za kufanyabiashara ya kuongoza watalii.

“Tunaiomba Kamisheni ya Utalii Zanzibar iweke masharti kwamba mtu anayetaka kufanya biashara hiyo apitie ZATO apitishwe kama anazosifa ndipo aende kupewa leseni, aje kwetu kwanza tumchuje kama anafaa na kama ni mtu asiyeaminika tueleze,” anasema.

Hassan anasema, licha ya ‘papasi’ kuvamia biashara hiyo, wako wageni wa kimataifa waliovamia biashara hiyo, ingawa sheria za Zanzibar, haiwaruhusu kufanya kazi hiyo.

Anasema, sheria inatamka kuwa biashara ya kuongoza watalii itafanywa na Wazanzibari na hivi sasa wageni wa mataifa mbalimbali, wamevamia na kufanya anachokitaja ‘vitu vya ajabu ajabu’ kwenye sekta hiyo hivyo kuwaathiri wao, ambao wamesajiliwa na wanalipa kodi zote serikalini.

“Wanafanya ‘ujanja ujanja’ mara mwingine anaingia kama mhudumu wa hoteli, mwingine anajifanya yeye ni mshauri mwelekezi wa fani fulani lakini ana ofisi yake mfukoni, anakaa na komyuta yake anafanyakazi hiyo, tumesema weee lakini hatua hazichukuliwi,” anasema Hassan.

Aidha, alisema umefika wakati mwafaka kamisheni hiyo ipitishe panga lake na kuwaondoa wageni wanaofanya biashara ya kuongoza watalii kwani fedha nyingi zinakwenda nje badala ya kubaki Zanzibar.

“Sisi wanachama wa ZATO tukifanya kazi hii fedha zinabaki hapahapa na tunatengeneza ajira kwa vijana wetu wa hapahapa lakini wenzetu hawa fedha zinarudi huko huko, sasa Sheria kwa kuwa ipo isimamiwe vizuri ili kazi hizi zifanywe na wazanzibari,” anasema

Hassan anaongeza iwapo Kamisheni ya Utalii itawaondoa ‘papasi’ na ‘beach boys’ kwenye biashara hiyo, idadi ya watalii itazidi kuongezeka na serikali itapata fedha nyingi.

“Tunaiomba Kamisheni ya Utalii (Zanzibar) itupe fursa ili kwa pamoja tudhibiti hii hali maana serikali itaendelea kupoteza kiasi kikubwa cha mapato kama ‘papasi’ na ‘beach boys’ wataachwa waendelee kutamba kwenye biashara hii, kamisheni ihakikishe kazi hii inafanywa na watu wenye utaalamu nayo tu,” anasisitiza

Anasema ni imani yao kuwa Kamisheni ya Utalii, itasikia ushauri wao ili waijenge Zanzibar kwa kuhakikisha wanarekebisha kasoro zilizopo na kuhakikisha ubabaishaji kwenye sekta hiyo unaondoshwa na serikali inapata stahiki yake ya mapato.

 

Habari Kubwa