Walemavu sasa waiangukia serikali

07Dec 2017
Peter Mkwavila
Nipashe
Walemavu sasa waiangukia serikali

SHIRIKISHO la vyama vya watu wenye ulemavu (Shivyawata), Mkoa wa Dodoma, limeiomba serikali kutenga bajeti na kutoa ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu ili viweze kutekeleza shughuli zao za kuwaletea maendeleo.

Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera, Bunge, kazi, ajira, vijana na watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama

Ombi hilo lilitolewa na Katibu wa shirikisho hilo, Justus Ng’wantalima, alipokuwa akizungumza juzi kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu yaliyofanyika mjini hapa.

Ng’wantalima, alisema serikali ikiwatengea bajeti hiyo na kutoa ruzuku watamudu na kutekeleza majukumu yao na kujiletea maendeleo ambayo yatawasaidia katika kuwapunguzia changamoto walizo nazo kwenye maisha yao ya kila siku.

Aliwataka viongozi wa ngazi mbalimbali zinazohusika katika kutoa uamuzi kuzingatia ili watu wenye ulemavu waweze kupatiwa fursa muhimu wanazostahiki kama ilivyo kwa watu wengine.

Alisema viongozi hao wasipozingatia kutoa maamuzi upande wao watu wenye ulemavu wataendelea kuwa mzigo kwa serikali na jamii inayowazunguka.

“Kitendo cha masuala ya watu wenye ulemavu kutozingatiwa na baadhi ya viongozi wenye mamlaka katika ngazi mbalimbali za maamuzi na jamii,bado watu hao wataendelea kukosa fursa muhimu wanazostahiki,”alisema.

Hata hivyo, alisema serikali inatakiwa kuhakikisha inawapatia bima ya afya watu wenye ulemavu maskini ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu,kwa ajili ya kuwawezesha kupata huduma hizo bila vikwazo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Cheshire Foundation, Dk.Steven Masangia, alisema wamekuwa wakiwawezesha ili waweze kujiajiri wenyewe kwa lengo la kukabiliana na maisha ndani ya jamii inayowazunguka.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.Binilith Mahenge, Ofisa Maendeleo ya Jamii,Wilaya ya Chamwino, Faraja Maduhu,alisema bado kuna tatizo kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu kutokana na kuwaficha na kuwakosesha haki zao za msingi.

Alisema serikali imeshatoa maamuzi yake kwa upande wa elimu kuhusu kusoma bure,hivyo hakuna sababu ya kutowapeleka watoto hao kupata haki zao za kimsingi kama ilivyo kwa watoto wengine. 

Habari Kubwa