Ongezeko la migodi chanzo uvamizi misitu

23Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ongezeko la migodi chanzo uvamizi misitu

ONGEZEKO la migodi midogo katika Halmashauri ya Mbogwe, wilayani hapa mkoani Geita, limetajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira katika hifadhi za misitu ya Bukombe Mbogwe na Moyowosi Kigosi kwa kukata magogo ya kuzuia migodi hiyo kutitia.

Ofisa Misitu wa Halmashauri ya Mbogwe, Emmanuel Bwai, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuwa wamekuwa wakipambana na wachimbaji wadogo wanaovamia hifadhi za misitu wasiendelee kuvamia na kukata magogo.

Alisema kuwa wachimbaji wadogo huvamia hifadhi za misitu za Moyowosi Kigosi na Bukombe Mbogwe na kukata magogo kwa ajili ya kuzuia kutitia kwa mashimo ya dhahabu pindi wanapokuwa katika shughulizao za uchimbaji na kuongeza jitihada zinazoendelea katika kuwapatia utaratibu wa upatikanaji wa magogo hayo.

Bwai alisema, zaidi ya hekta 30 zimevamiwa na kuvunwa na wachimbaji wadogo huku 25 zikivunwa kutoka katika hifadhi za misitu ya serikali na hekta tano zikivunwa kutoka katika moja ya hifadhi za misitu ya watu binafsi.

Alisema halmashauri imekuwa ikiwachukulia hatua wote wanaohusika na kukutwa na magogo bila kibali.

Aidha, alitaja machimbo wanayoyazungukia na kukagua magogo yanayovunwa kinyume na sheria za uhifadhi za misitu kuwa ni Nyakafuli, Nyarubenzi, Bukande, Kakambi, Shenda, Bukanga, Kanegele, Nyakasuluma na Shikambuga.

“Tumekuwa tukiwakamata na kuwafikisha mahakamani wote wanaovamia misitu na kuvuna magogo, tulikuwa na kesi tano za uvamizi wa hifadhi wa misitu, mbili ziliamuliwa na mahakama moja inaendelea kusikilizwa na mbili bado zipo katika upelelezi, lengo ni kuwakamata na kuwafikisha mahakamani,” alisema Bwai.

Ofisa Mazingira wa halmashauri hiyo, Charles Tui, alisema wameanza kuwapatia elimu wachimbaji wadogo namna ya kutumia nondo kudhibiti mashimo yao kutiti.

Alisema shughuli za kilimo zimesababisha uvamizi mkubwa katika maeneo ya hifadhi kwa kuongeza maeneo ya kilimo sambamba na wafugaji kuvamia na kufyeka maeneo ya kutunzia mifugo yao.

Alisema halmashauri imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kutoa elimu kwa wafugaji, wavamizi wa hifadhi ili wasiendelee kuvamia maeneo hayo.

Alisema wamekuwa wakitekeleza agizo la serikali la kila halmashauri kupanda miche ya miti milioni 1.5 huku katika shule za msingi na sekondari pamoja na taasisi za kiserikali na watu binafsiwakipanda miche 40,000. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbogwe, Elias Kayandabila, alisema halmashauri imetenga Sh. milioni 10 kupambana na wavamizi. 

Habari Kubwa