Akoleza ufugaji wa nyuki

23Feb 2018
Cynthia Mwilolezi
Nipashe
Akoleza ufugaji wa nyuki

WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia misitu kufuga nyuki kwa ajili ya asali itakayowaongezea kipato na kupiga vita umaskini.

Akizungumza jijini katika kongamano la wataalam wa ufugaji nyuki toka mataifa sita duniani, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, alisema misitu iliyopo hasa maeneo ya vijijini bado ni fursa kubwa kwa wananchi kujiongezea kipato.

“Vijijini kuna misitu ya kutosha, wananchi wakiitumia vizuri kufugia nyuki watapata asali itakayouzwa soko la ndani na nje ya nchi. Asali imekuwa zao linalochangia uchumi wa taifa, mpaka sasa imechangia Sh. bilioni 3.8,” alisema.  

Alisema ingawa Tanzania ina misitu mingi, lakini uchunguzi umebaini ni asilimia 10 tu inayotumika kwa ufugaji nyuki.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Cesosaco la Canada, likishirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) na Wizara ya Maliasili na Utalii, lilitoa fursa ya majadiliano ya namna asali kuboreshwa na kuwezesha wananchi kuondokana na umaskini.

Mkurugenzi wa mafunzo na huduma za mikoa kutoka Sido, Joyce Meru, alisema, ili kuzalisha asali kwa ufanisi zaidi ipo haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji nyuki na wakusanya asali.

“Bado asali inazalishwa kwa kiwango cha chini kutokana na kukosa elimu ya namna ya kuzalishwa, ufungashaji na kujua soko liko wapi…hayo yote yanatoa fursa ya kuzidi kufundisha namna ya kuifahamu sekta hiyo zaidi,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Sido, Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji,  alisema kongamano hilo liliandaliwa kwa ajili ya kuangalia uzalishaji wa mazao ya nyuki yanaweza kuongezeka.

“Jukumu letu ni kuhakikisha wajasiriamali wanatoka hapo walipo kwenda juu kwa maana ya kuzalisha asali na nta yenye ubora ikiwamo kupata masoko ya ndani na nje ya nchi,” alisema.

Nchi zilizoshiriki katika kongamano hilo ni Tanzania, Canada, Philippine, Bolivia, Senegal, Ethiopia na Burkina Faso.

 

 

Habari Kubwa