Taifa Stars msikate tamaa

12Jun 2017
Mhariri
Nipashe
Taifa Stars msikate tamaa

JUZI timu yetu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) ilicheza mchezo wake wa kwanza wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Afrika zitakazofanyika mwaka 2019.

Katika mchezo huo dhidi ya Lesotho, Stars ililazimishwa sare ya bao 1-1 mchezo huo ulichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Nipashe tunaamini matokeo haya hayakuwa mzuri sana kwa Stars ambao walipaswa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani na kujikusanyia pointi tatu na mabao zaidi ambazo zingewapa nguvu kuelekea kwenye mchezo mwingine wa kundi lao lenye timu nne.

Stars ina kazi nyingine mbele yao watakapoumana na Uganda na Cape Verde kwenye kundi lao ambalo linaonekana kuwa gumu.

Pamoja na matokeo waliyoyapata Stars, tunaamini bado timu hiyo ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zijazo za kundi lao.

Cha msingi ni benchi la ufundi la Stars lililo chini ya Kocha Salum Mayanga linapaswa kufanyia kazi mapungufu waliyoyaona kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Lesotho.

Matokeo ya mchezo uliopita yasiwavuruge wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo bali wachukulie kama changamoto na wajipange kwa michezo ijayo.
Mchezo dhidi ya Lesotho umepita na kwa sasa mipango inatakiwa kuandaliwa mapema kujiandaa na mchezo ujao utakaochezwa dhidi ya Uganda.

Tunaamini makocha wa Stars wameyaona mapungufu yaliyopelekea kulazimishwa sare na Lesotho, hivyo ni vyema sasa Mayanga na makocha wenzake kuyafanyia kazi mapema mapungufu hayo ni ikiwezekana timu icheze michezo ya kirafiki kabla ya kucheza mchezo mwingine wa kundi lao.

Kucheza mchezo wa kirafiki kutamsaidia Mayanga kugundua mapungufu ya timu na kuyafanyia kazi mapema kabla ya mchezo mwingine wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Afrika za mwaka 2019.

Tunawakumbusha wachezaji wa Taifa Stars kutokata tamaa, badala yake wajipange kwa ajili ya michezo mingine iliyoko mbele yao na kupeperusha vyema bendera yaTaifa letu.

Kila panapokuwa na nia ya dhati, maendeleo yanapatikana, hivyo wachezaji kama wataka kuipeleka Tanzania kwenye fainali zijazo za Afrika, wanapaswa kupambana na kuwa na nia ya dhati.

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kwa nafasi yao wanajitahidi kuiandaa timu, lakini pia peke yao hawawezi, kwa kuwa timu sio klabu ni timu ya taifa, kila Mtanzania kwa nafasi yake hasa wadau wa soka wanapaswa kuisaidia kwa namna mbalimbali timu yetu kwa kuwa ndiyo inayopeperusha bendera ya taifa letu.

Hivi karibuni, TFF iliipeleka Stars kwenye kambi ya wiki moja nchini Misri kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa juzi dhidi ya Lesotho, juhudi hizo za TFF zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote wa soka nchini.

Mafanikio ya Taifa Stars ni mafanikio ya kila Mtanzania, na sisi kama wadau wa soka tungependa kuona Taifa Stars inashiriki fainali zijazo za Afrika.

Ikumbukwe Tanzania ina zaidi ya miaka 36 haijashiriki fainali za Afrika tangu ilipofanya hivyo mwaka1980, ni vyema sasa tukaweka mkazo kwenye michezo hii ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Afrika.

Tunawaomba wachezaji na benchi la ufundi la Taifa Stars wasikate tamaa na matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho bali wajipange sasa kwa ajili ya mchezo ujao wa kundi lao.

Ni matarajio yetu pia kuwa mdhamini wa Taifa Stars, Serengeti Breweries wataendelea kuisaidia timu hiyo ikiwamo kuiwezesha kukaa pamoja kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi dhidi ya timu zilizoko katika kundi lake.

Habari Kubwa