Wapendekeza mahakama kutoa vifungo kukomesha migogoro

Ndikilo aliyasema hayo juzi wilayani hapa wakati akihitimisha ziara yake katika wilaya sita za mkoa wa Pwani.

Alisema migogoro hiyo haina tija baina ya makundi hayo mawili, hivyo hawapo tayari kuendelea kufumbia macho matukio hayo.

Ndikilo alisema katika kukomesha matukio hayo wamepanga kuongea na mhimili unaohusika ili watuhumiwa wa matukio hayo wanapofikishwa mahakamani na kupatikana na hatia wapewe adhabu za vifungo badala ya kupigwa faini.

Alisema wafugaji wanapofikishwa mahakamani na kupatikana na hatia na kisha kupigwa faini wanamudu kulipa hali inayowafanya kuendelea kuwa na kiburi cha kuendeleza migogoro hiyo.

Akizungumzia suala la ulinzi na usalama, aliwataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kuacha kuamini wageni wanaoingia katika maeneo yao.

“Ukiona kuna mtu yupo kijijini ama kwenye mtaa wako humjui na unamtilia shaka, toeni taarifa kwenye vyombo vya dola ili viweze kuchukua hatua," alisema Ndikilo.

Katika hatua nyingine aliwataka wazazi na walezi kusomesha watoto wao wa kike na wakiume bila kuwabagua kutokana na elimu ni ufunguo wa maisha yao ya baadae.