Wadau: Sera ya Utalii imepitwa na wakati

14May 2017
George Tarimo
Nipashe Jumapili
Wadau: Sera ya Utalii imepitwa na wakati

SERIKALI imesema inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza watalii kwa kuweka vivutio vingi zaidi ikiwamo kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege eneo la Nyanda za Juu Kusini.

Wakizungumza kwenye mkutano baina ya wadau wa sekta hiyo, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Wizara ya Maliasili na Utalii, uliofanyika mjini Iringa mwishoni mwa wiki, baadhi ya wadau hao walisema licha ya Sera ya Utalii ya mwaka 1999, kupitwa na wakati, miundombinu mibovu pamoja na utitiri wa kodi kwenye sekta hiyo ni kikwazo kwa maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Wadau wa utalii, Alban Lutambi na Joseph Kisanyage, walisema kwa sasa  hifadhi zote tano za kusini hakuna zenye barabara nzuri.

Mshauri mwelekezi aliyeteuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kufanyia marekebisho Sera ya Utalii ya mwaka 1999, Prof. Raphael Mwalyosi, alisema sera hiyo imepitwa na wakati kwa kuwa pamoja na mambo mengine imeshindwa kutambua vivutio vingi vya utalii hasa ambavyo haviko chini ya wizara hiyo pia ikiacha taasisi nyingi kujipangia kodi za utalii na kusababisha utitiri wa kodi.

Mwalyosi alisema Hifadhi ya Taifa (TANAPA) wanazungumzia juu ya hifadhi za taifa, mamlaka ya Ngorongoro wanazungumzia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa hiyo maeneo yaliyo nje hawana mtu wa kuwazungumzia.

Alisema, licha ya taasisi nyingi zinazohusika na mambo ya utalii, kuna kodi nyingi kwa sababu kila moja ina kodi zake hadi kufikia 56.

Naye  Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii, Zahoro Kimwaga, alisema Sera ya Utalii ya mwaka 1999, inatakiwa kufanyiwa marekebisho ili iweze kushirikisha sekta binafsi katika kuifanya Sekta ya Utalii inayoongoza kuliingizia taifa fedha za kigeni na kutoa ajira zaidi ya milioni 1.5.

Akizungumzia upungufu katika sera hiyo, alisema imechukua takribani miaka 17 na kwa kawaida sera nyingine zinachukua miaka 10.

Alisema ipo haja ya kuipitia sera hiyo mpya ili kuhakikisha ushirikishwaji wa wadau hao upo wazi na unaeleweka.

Alisema kuwa kwa taarifa walizonazo tangu mwaka 2012 hadi 2015 imechangia zaidi ya aslimia 25 ya pato la taifa na pia kuongeza mapato ya dola za kimarekani dola Bil.1712 kwa mwaka 2012 hadi kufikia dola za kimarekani dola 1901 kwa mwaka 2015.

Habari Kubwa